Msanii Kareh B avunja kimya baada ya kumzika mwanawe aliyefariki kwenye ajali ya Chavakali

Kareh B amebainisha kuwa alipata sapoti isiyoyumba wakati wa majonzi na akamshukuru kila mtu aliyekuwapo kwa ajili yake.

Muhtasari

•Kareh B ametoa shukrani zake za dhati kwa kila mtu ambaye amemuonyesha upendo na sapoti katika nyakati hizi za huzuni.

•Kareh B aliendelea kuorodhesha watu kadhaa mashuhuri ambao walionyesha sapoti kubwa kwake na familia yake.

Image: FACEBOOK// KAREH B

Malkia wa Mugithi Mary Wangari Gioche almaarufu Kareh B, ambaye hivi majuzi alimpoteza mwanawe  ametoa shukrani zake za dhati kwa kila mtu ambaye amemuonyesha upendo na sapoti katika nyakati hizi za huzuni.

Mwanawe Kareh B mwenye umri wa miaka 17,  Joseph Mwadulo alipoteza maisha katika ajali ya barabarani iliyotokea mnamo Aprili 1 baada ya basi alilokuwa akisafiria kuanguka katika eneo la Mamboleo Junction, kaunti ya Kisumu. Mwanafunzi huyo wa kidato cha nne alikuwa akisafiri kwenda nyumbani pamoja na wanafunzi wenzao walipohusika katika ajali hiyo.

Katika taarifa yake ya Jumapili asubuhi, mwimbaji huyo wa mugithi alibainisha kuwa alipata sapoti isiyoyumba wakati wa majonzi na akamshukuru kila mtu aliyekuwapo kwa ajili yake.

"Wapendwa Marafiki, sikuwahi kujua kuwa nina familia kubwa sana ambayo naweza kutegemea, natamani ningewataja nyote kwa majina lakini orodha haina mwisho ❤️❤️," Kareh B alisema kupitia ukurasa wake wa Facebook.

Aliongeza, “Nataka kuchukua muda kuelezea shukrani zangu za dhati kwa kutia moyo kwako bila kuyumbayumba wakati wa kumtuma mwanangu kwa “Dulo”. Uwepo wako na fadhili ulimaanisha ulimwengu kwangu katika wakati huu mgumu. Asante kwa kuwa huko kutoa maombi, faraja na nguvu. Usaidizi wako umefanya mabadiliko makubwa katika maisha yangu, na ninashukuru sana.”

Kareh B aliendelea kuorodhesha watu kadhaa mashuhuri ambao walionyesha sapoti kubwa kwake na familia yake akiwemo naibu rais Rigathi Gachagua, gavana Mutahi Kahiga, Mbunge Kimani Ichung’wah, mwimbaji Jose Gatutura, miongoni mwa wengine.

Joseph Mwadulo, mwana wa mwimbaji Mugiithi KarehB alizikwa, nyumbani kwa mzazi wake huko Kimangaru, Kaunti ya Embu mnamo Aprili 12.

Mwadulo ambaye alikuwa ni mwanafunzi wa shule ya upili ya Chavakali kaunti ya Vihiga alifariki kwenye ajali. Ajali hiyo ilitokea katika makutano ya Mamboleo kaunti ya Kisumu mnamo Aprili 1, 2024.

Ibada ya mazishi ya Mwanafunzi wa Shule ya Upili ya Chavakali Joseph Mwadulo mnamo Ijumaa, Aprili 12, 2024. 

Waombolezaji walikutana katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Chuo Kikuu cha Kenyatta kabla ya kuelekea Embu kwa ibada ya kanisa na kisha kuelekea eneo la maziko.

Sherehe ya mazishi ilihudhuriwa na familia, marafiki, walimu, na wanafunzi wa Shule ya Upili ya Wavulana ya Chavakali ambapo mtoto huyo wa miaka 17 alikuwa akisoma.

 Watu maarufu waliohudhuria ni pamoja na Jacque Nyaminde - Wilbroda Shirandula, Nyambura Wa Kabue, Shix Kapienga - Tasha, Wanjiku The Teacher, Njeri ithaga riene, Jose Gatutura, Terence Creative, Kamoko Wanjiru Waya Joyce na Wamamaa Wanja asali Mtoto wakiambulia. Mwadulo alipata ajali ya barabarani akitokea shuleni.