Zakayo ni jina, bora tulipe ushuru- Ruto asema

"Kuitwa Zakayo sio shida. Bora tulipe Ushuru. Zakayo ni jina. Hakuna tatizo tunaweza kusonga mbele," Rais alisema.

Muhtasari

•Ruto amesema hana wasiwasi wowote kuhusu kuitwa Zakayo mradi Wakenya walipe ushuru utakaomsaidia kubadilisha nchi.

•Jina la Zakayo liliibuka kwenye mitandao ya kijamii baada ya utawala wa Ruto kuzindua ushuru mpya kama vile ushuru wa nyumba.

wakati wa Sherehe za Siku ya Wafanyakazi katika bustani ya Uhuru mnamo Jumatano, Mei 1, 2024.
Rais William Ruto wakati wa Sherehe za Siku ya Wafanyakazi katika bustani ya Uhuru mnamo Jumatano, Mei 1, 2024.
Image: PCS

Rais William Ruto amesema hana wasiwasi wowote kuhusu kuitwa Zakayo wa Kibiblia mradi Wakenya walipe ushuru utakaomsaidia kubadilisha nchi.

Akihutubia hafla ya 59 za Siku ya Wafanyakazi katika bustani ya Uhuru Gardens, Nairobi, Rais alisema lazima Wakenya wawe tayari kujenga taifa lao kupitia rasilimali zao na wala si madeni.

Ni wakati akitoa matamshi hayo ambapo alirudia, tena, kwamba kuitwa Zakayo wa Kibiblia halikuwa tatizo kwake.

"Kuitwa Zakayo sio shida. Bora tulipe Ushuru. Zakayo ni jina. Hakuna tatizo tunaweza kusonga mbele," Rais alisema.

"Bora tujenge Kenya hii; watu wapate nyumba, tuwe na universal health coverage na watoto wetu wapate ajira, Zakayo ni jina tuendelee mbele."

Jina la Zakayo liliibuka kwenye mitandao ya kijamii baada ya utawala wa Ruto kuzindua ushuru mpya kama vile ushuru wa nyumba.

Sehemu ya Wakenya waliochukizwa walilinganisha hatua zake za ushuru na zile za Zakayo wa kibiblia, ambaye alikuwa mtoza ushuru huko Yeriko.

Lakini mkuu wa taifa mara nyingi amekuwa akidhihaki majina hayo katika onyesho dhahiri la kutokuwa na shida na jina hilo.

Akizungumza mjini Tokyo mwezi Februari, Rais alisema licha ya kuitwa majina mbalimbali nyumbani atasimamia maamuzi yake madhubuti ya kuiweka nchi kwenye njia sahihi.

"Sijali watu wakiniita kwa majina. Nitaendelea kufanya mambo yanayofaa kwa nchi yetu bila kujali majina ambayo watu wananiita akiwemo Zakayo," Ruto alisema.

Mkuu huyo wa nchi aliongeza kuwa unapofanya jambo sahihi, dhamiri yako huwa safi.