Tanzania na Kenya zasuluhisha mzozo wa mauzo ya kuku baada ya miaka mitatu

Mwaka 2018 Tanzania ilichoma vifaranga 5,000 vya kuku vilivyodaiwa kuingizwa nchini humo kutoka Kenya.

Muhtasari

•Mzozo huo ulitatuliwa wakati wa mkutano wa mashauriano wa siku mbili uliofanyika makao makuu ya kaskazini mwa Tanzania jijini Arusha uliomalizika Jumanne.

Image: BBC

Tanzania na Kenya zimefanikiwa kutatua mgogoro wa muda mrefu wa mauzo ya kuku na bidhaa za kuku baina ya nchi hizo mbili, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ilisema katika taarifa yake Jumanne.

Taarifa hiyo ilisema mzozo huo ulitatuliwa wakati wa mkutano wa mashauriano wa siku mbili uliofanyika makao makuu ya kaskazini mwa Tanzania jijini Arusha uliomalizika Jumanne.

Mwenyekiti mwenza wa mkutano huo Rabson Wanjala, kutoka Kenya ambaye alimuwakilisha Balozi wa Kenya nchini Tanzania, alisema nchi zote mbili zimejitolea kukuza uhusiano wa kibiashara, na kuongeza kuwa ahadi zao zinasisitiza juu ya umuhimu wa juhudi za ushirikiano ili kuhakikisha biashara inaongezeka katika ukanda huo.

Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo Wizara ya Mifugo na Uvuvi nchini Tanzania Benezeth Lutege Malinda amesema Tanzania inashughulikia kikamilifu vikwazo vya kibiashara kwa kuhakikisha mashirika yote yanayowezesha biashara yanajikita katika kutatua masuala hususani vikwazo visivyo vya ushuru vinavyokwamisha biashara.

"Tunaendelea kujitolea kukabiliana na changamoto hizi na kukuza mazingira mazuri ya biashara kati ya Kenya na Tanzania," alisema.

Mwaka 2018 Tanzania ilichoma vifaranga 5,000 vya kuku vilivyodaiwa kuingizwa nchini humo kupitia mpaka wa Kaskazini wa Namanga kutoka Kenya.