Watalii wakwama katika mbuga la Maasai Mara kutokana na mafuriko

Pia kuna hofu kuwa huenda baadhi ya wanyama walisombwa na mafuriko hayo.

Muhtasari

•Zaidi ya nyumba 10 za kulala wageni na kambi zimefurika baada ya Mto Talek ulio karibu kuvunja kingo zake siku ya Jumanne.

Image: BBC

Watalii wanahamishwa kutoka mbuga maarufu ya Maasai Mara nchini Kenya baada ya mafuriko kukumba sehemu kubwa ya mbuga hiyo.

Zaidi ya nyumba 10 za kulala wageni na kambi zimefurika baada ya Mto Talek ulio karibu kuvunja kingo zake siku ya Jumanne.

Pia kuna hofu kuwa huenda baadhi ya wanyama walisombwa na mafuriko hayo.

 

Mkuu wa polisi wa eneo hilo, Kipkoech Lotiatia, aliambia BBC kuwa hifadhi hiyo iliharibiwa vibaya.

"Maji yamepungua lakini baadhi ya nyumba za kulala wageni na kambi bado ziko chini ya maji," Bw Lotiatia alisema.

Haijulikani ni watu wangapi wamenaswa katika hifadhi hiyo, lakini takriban 36 wameokolewa hadi sasa kwa ndege na wengine 25 na timu ya uokoaji ya mashua, Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya lilisema.

"Katika baadhi ya kambi, mahema yamesombwa na maji, na daraja la Mara, linalounganisha Mara Trianglena Greater Mara, limesombwa na maji," shirika hilola misaada liliongeza.

Watalii wengi wa kigeni na wa ndani hutembelea hifadhi hiyo kujionea wanyamapori wake wakiwemo simba, chui na duma.

Bw Lotiatia awali aliwaambia wanahabari kwamba timu za uokoaji zilikuwa zikitumia helikopta mbili za dharura kuwahamisha watalii na wafanyikazi.

Uongozi wa Masai Mara haukujibu mara moja ombi la BBC la kutaka maoni yao.

Mto Talek ulipasua kingo zake Jumanne alasiri kufuatia mvua kubwa iliyonyesha juu ya mto huo.

Hali imekuwa mbaya zaidi kutokana na maji yanayotiririka kutoka mto Mara, karibu na mpaka wa Serengeti na Tanzania, kufuatia mvua nyingi katika eneo hilo.

"Baada ya siku kadhaa za mvua zinazoendelea kunyesha, mito yetu imejaa maji, na kuathiri kambi na maeneo kadhaa katika Hifadhi ya Kitaifa ya Maasai Mara," serikali ya kaunti ya Narok ilisema kupitia taarifa.

Barabara na madaraja pia yamezamishwa na maji, na kuathiri jamii zinazoishi huko.