Mafuriko Kenya: Baadhi ya nyumba za Nairobi zabomolewa huku Kimbunga Hidaya kikikaribia

Kote katika Kaunti ya Nairobi, mamia ya watu wameshuhudia nyumba zao zikibomolewa.

Muhtasari

•Ubomoaji huo unafuatia agizo la serikali kwa mtu yeyote anayeishi karibu na mito kuacha makazi yake na kuhamia maeneo ya juu.

•msemaji wa serikali Isaac Mwaura alisema: "Hawa ni watu walewale wanaokufa. Hawa ni watu ambao wanaathirika na mafuriko haya.

Image: BBC

Mabaki ya vyuma vilivyosukwa, vipande vikubwa vya mbao na magodoro ambayo hayakuwekwa sawa ni mabaki ya yale yaliyokuwa makazi ya watu katika mtaa wa mabanda wa Mukuru wa Reuben katika mji mkuu wa Kenya.

Kote katika Kaunti ya Nairobi, mamia ya watu pia wameshuhudia nyumba zao zikibomolewa.

Ubomoaji huo unafuatia agizo la serikali kwa mtu yeyote anayeishi karibu na mito kuacha makazi yake na kuhamia maeneo ya juu baada ya mvua kubwa na mafuriko, ambayo yameathiri eneo la Afrika Mashariki kwa wiki kadhaa.

Vitongoji duni vinaunda sehemu kubwa ya vitongoji vilivyojengwa kwenye ardhi ya kando ya mabonde ya mito.

Serikali imesema ubomoaji huo ulikuwa muhimu ili kuzuia vifo zaidi. Pia ilisema kuwa kuishi ndani ya mita 40 kutoka kwenye kingo za mto ni kinyume cha sheria.

Hapo awali, mamlaka iliwapa watu katika maeneo yaliyotengwa saa 24 kuhama, tarehe ya mwisho ambayo iliisha Ijumaa jioni.

Hata hivyo, wakazi wengi waliiambia BBC kwamba walipatwa na mshangao kwamba nyumba zao zilibomolewa kabla ya muda uliowekwa

Nicholas, mfanyakazi wa kawaida, alifika nyumbani kutoka kazini na kukuta nyumba yake ikiwa imeharibika.

Akiwa bado na mshtuko, alisema: "Inauma sana. Walipaswa kutupa muda wa kupata pesa na kufikiria jinsi ya kujipanga angalau.

"Lakini kutupa taarifa fupi, na tunafanya kazi, sio haki hata kidogo."

Kama Nicholas, mama wa watoto wawili Phylis alisema alikuwa akijaribu kujua mahali pa kwenda na jinsi ya kusafirisha mali ambayo alifanikiwa kuokoa.

"Nina watoto, hawajala chochote. Mimi ni mama ninayelea watoto peke yangu... wameharibu maisha yetu," anasema kwa hasira.

Image: BBC

Walioshuhudia ubomoaji huo waliiambia BBC kuwa jeshi lilihusika, huku picha zilizochapishwa na vyombo vya habari zikionekana kuonesha wanaume wakiwa wamevalia mavazi ya kijeshi wakisimamia uvunjaji huo. Jeshi halijatoa maoni yoyote.

Lakini msemaji wa serikali Isaac Mwaura alisema: "Hawa ni watu walewale wanaokufa. Hawa ni watu ambao wanaathirika na mafuriko haya.

"Wakati mwingine maji yanapopungua basi watu wanarudi kwenye majengo yao. Kwa hiyo kama serikali inabidi tuwe wazi sana na dhahiri."

Ingawa sehemu za Mukuru Wa Reuben zimeharibiwa, na licha ya maonyo ya mafuriko, wakazi kama Nicholas walisema watapiga kambi karibu na nyumba zao zilizoharibiwa Ijumaa usiku kwani hawana mahali pengine pa kwenda.

Image: BBC

Serikali inasema imewahamisha watu chini ya 27,600 waliolazimishwa kutoka kwenye makazi yao na mafuriko katika kambi mpya zilizojengwa.

Takribani watu 210 kote nchini wamefariki kutokana na mafuriko hayo, huku wengine 90 wakiwa hawajulikani walipo, kulingana na makadirio rasmi ya hivi karibuni. Wiki hii tu, zaidi ya watu 50 walipoteza maisha wakati wa wimbi la maji lilipopitia vijiji karibu na mji mkuu, Nairobi.

Mvua kubwa inatabiriwa kuendelea kwa mwezi mzima na mabwawa 178 yana hatari kubwa ya kufurika, mamlaka imeonya.

Zaidi ya hayo, Rais William Ruto ameonya taifa huenda likakumbwa na kimbunga cha kwanza kabisa, huku Hidaya kikizidi kushika kasi katika pwani ya Tanzania siku ya Ijumaa.

Katika hotuba ya runinga, aliamuru shule zifungwe kwa muda usiojulikana.

Katika nchi jirani ya Tanzania, msemaji wa serikali Mobhare Matinyi aliiambia BBC kuwa mamlaka iko katika hali ya kusubiri na iko tayari kuwahamisha watu wanaoishi katika maeneo ya pwani yaliyo hatarini kutokana na kimbunga hicho, ambacho kinaweza kulikumba jiji kubwa zaidi la Dar es Salaam.

Wakazi wamehimizwa kuchukua tahadhari.

Maeneo mengine ambayo huenda yakaathiriwa na kimbunga hicho ni pamoja na Mtwara, Lindi, Tanga na Zanzibar.

Mamlaka ya hali ya hewa nchini, TMA ilisema Ijumaa kwamba kimbunga hicho kilitarajiwa kusababisha mvua kubwa na upepo mkali. Takribani watu 160 wamefariki kutokana na mafuriko nchini humo.

“Tunataka watu wote wanaofanya shughuli za baharini na wasafirishaji kuchukua tahadhari, na kufuata ushauri kutoka kwa shirika la utabiri wa hali ya hewa ili kupunguza hatari,” alisema Bw Matinyi.

Siku ya Ijumaa mchana, maduka na biashara zilizo karibu na bahari jijini Dar es Salaam zilikuwa zikifanya kazi kawaida lakini baadhi ya watu walisema wanarudi nyumbani mapema kwa sababu ya hatari ya kunyesha kwa mvua kubwa.

Safari za Dar es Salaam kuelekea visiwa vya Zanzibar zimesitishwa kutokana na hali mbaya ya hewa, pia huduma za kivuko kuelekea maeneo ya Kigamboni Dar es Salaam zimesimama.

Huko Nairobi, Phylis, ambaye tayari amelazimika kuondoka nyumbani kwake, alihimiza mamlaka kuwa na mpango thabiti linapokuja suala la kuhama.

"Serikali ikitubomolea nyumba angalau itupe suluhu, watuambie tuelekee wapi, hatujui pa kwenda," alisema.