228 wamefariki, 72 hawajulikani waliko huku mvua ya wastani hadi kubwa ikitarajiwa katika kaunti 37

Maeneo yatakayoathirika ni Pwani, Magharibi, maeneo ya Ziwa Victoria, Kati, Mashariki, Bonde la Ufa na Nairobi.

Muhtasari

•Wizara ya Masuala ya Ndani imesema jumla ya boma 42,526 zimehamishwa na takriban watu 227,238 wameathiriwa na mvua kubwa inayoendelea.

•Maeneo mengi ya Turkana, Samburu, Marsabit, Isiolo, Garissa, Wajir, Mandera, Taita Taveta na Tana River yanatabiriwa kuwa kavu kwa ujumla.

Mafuriko nchini Kenya
Image: BBC

Takriban vifo 228 vimeripotiwa, watu 164 wamejeruhiwa na 72 bado hawajulikani walipo kufikia sasa huku mvua kubwa ikiendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini.

Wizara ya Masuala ya Ndani inayoongozwa na waziri Kindiki Kithure imesema jumla ya boma 42,526 zimehamishwa na takriban watu 227,238 wameathiriwa na mvua kubwa inayoendelea.

Hii ni wakati mvua ya wastani hadi kubwa ikitarajiwa kunyesha katika kaunti 37 za Kenya. Maeneo yatakayoathirika ni Pwani, Magharibi, maeneo ya Ziwa Victoria, Kati, Mashariki, Bonde la Ufa na Nairobi.

 

Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Ndani; kaunti za Kwale, Mombasa, Kilifi, Lamu, Kakamega, Vihiga, Busia, Bungoma, Trans Nzoia, Kisumu, Kisii, Nyamira, Migori, Siaya, na Homabay zimetabiriwa kukumbwa na mvua za wastani hadi kubwa zilizoambatana na radi mnamo Jumapili, Mei 5.

Kaunti zingine zitakazoathirika ni pamoja na; Nyeri, Murang’a, Kirinyaga, Kiambu, Nyandarua, Machakos, Kitui, Makueni, Embu, Tharaka Nithi, Meru, Nandi, Bomet, Narok, Kajiado, Uasin Gishu, Nakuru, Laikipia, Elgeyo Marakwet, West Pokot, Baringo, na Nairobi.

Mafuriko yanatarajiwa katika maeneo ya tambarare, maeneo ya pembezoni na maeneo ya mijini huku maporomoko ya ardhi yakatokea katika maeneo yenye miteremko mikali, miinuko na mikondo ya maji.

Maeneo mengi ya kaunti za Turkana, Samburu, Marsabit, Isiolo, Garissa, Wajir, Mandera, Taita Taveta na Tana River yanatabiriwa kuwa kavu kwa ujumla.

Hata hivyo, mvua kubwa inayoendelea kunyesha katika eneo la Kati na kufurika kwa Mabwawa ya Seven Forks kunaweza kusababisha mafuriko katika eneo la Tana Delta na hivyo kuathiri Kaunti za Garissa, Tana River na Lamu.

Wizara ya mambo ya ndani pia imetangaza kuwa kimbunga Hidaya ambacho kilikuwa kimetangazwa hapo awali kimeisha na kinatabiriwa kuwa kimedhoofika. Eneo la pwani hata hivyo bado litapata mvua kubwa yenye upepo mkali na mawimbi makubwa.

Katika saa 24 zilizopita, mafuriko yameshuhudiwa katika maeneo ya Marsabit, Tharaka Nithi, Baringo, Kisumu, Machakos, Nakuru, Uasin Gishu, Busia, Laikipia, Nyandarua, Trans Nzoia, Nairobi, Wajir, Mandera, Bomet, Kajiado, Embu, na Nyeri.

Maporomoko ya ardhi na matope yalitokea katika kaunti za Pokot Magharibi, Elgeyo Marakwet, Kericho, na Makueni.