Kenya yatafuta Bilioni 720 za kuunganisha SGR kutoka Naivasha hadi Malaba

Murkomen alisema sehemu zilizosalia za SGR kutoka Naivasha nchini Kenya hadi Uganda, Rwanda, Sudan Kusini na DRC, zitakamilik

Muhtasari

•Murkomen anasema hatua hiyo pia itaunda maeneo maalumu ya kiuchumi kando ya ukanda huo na kubadilisha miji ambayo maeneo ya kiuchumi yatakuwa.

Image: BBC

Kenya inataka kuimarisha ushirikiano wa sekta binafsi ili kupanua Reli ya Standard Gauge (SGR), ili kuhakikisha usafirishaji wa bidhaa unavuka mpaka bila matatizo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Waziri wa Barabara na Uchukuzi wa Kenya Kipchumba Murkomen anasema hatua hiyo pia itaunda maeneo maalumu ya kiuchumi kando ya ukanda huo na kubadilisha miji ambayo maeneo ya kiuchumi yatakuwa.

Akizungumza mjini Mombasa katika mkutano wa mawaziri, Murkomen alisema sehemu zilizosalia za SGR kutoka Naivasha nchini Kenya hadi Uganda, Rwanda, Sudan Kusini na DRC, zitakamilika, na kwamba wameandaa ramani ambayo itaharakisha utekelezaji wake.

"Lengo kuu chini ya Mtandao wa Miundombinu ya Kiafrika ni kuhakikisha tunaunganisha Pwani ya Mashariki hapa Mombasa na Pwani ya Magharibi kupitia Duala nchini Cameroun tunatamani kuhakikisha kuwa mawasiliano yanafanyika hadi DRC," Alisema Murkomen.

"Ninaamini kwamba ndoto ya SGR ipo na tunataka kuitimiza haraka. Tunataka kuinua sekta binafsi na ninajua mradi tulio nao sasa kutoka Naivasha hadi Malaba ikijumuisha uboreshaji karibu na Bandari ya Kisumu unakadiriwa kugharimu nchi takribani dola bilioni 5.3 (Ksh.700.3 bilioni)’' Alisema.