Watu kadhaa hawajulikani walipo baada ya maporomoko ya ardhi Kimende

Shirika la Msalaba Mwekundu limesema hakuna vifo vilivyoripotiwa lakini hata hivyo kuna watu ambao hawajajulikana waliko.

Muhtasari

•Watu kadhaa hawajulikani waliko baada ya maporomoko ya ardhi kutokea Jumanne usiku katika eneo la Kimende, kaunti ya Kiambu.

•Hapo awali walikuwa wamefichua kuwa timu ilikuwa imetumwa katika eneo la tukio kusaidia watu walioathirika.

Picha ya maktaba ya maporomoko ya ardhi
Image: MAKTABA

Watu kadhaa wanaripotiwa kutojulikana waliko baada ya maporomoko ya ardhi kutokea siku ya Jumanne usiku katika eneo la Kimende, kaunti ya Kiambu.

Kulingana na shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya, tukio hilo lilitokea Miteremko ya Kimende.

Katika taarifa ya mwisho ya Jumanne jioni, shirika hilo liliripoti kuwa hakuna vifo vilivyoripotiwa lakini hata hivyo kuna watu kadhaa ambao hawajajulikana waliko.

"Viwanja vimezingirwa na kutangazwa eneo la hatari. Ingawa hakuna vifo vilivyothibitishwa, watu kadhaa bado hawajulikani waliko,” shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya lilisema kwenye taarifa iliyochapishwa kwenye Twitter.

Hapo awali walikuwa wamefichua kuwa timu ilikuwa imetumwa katika eneo la tukio kusaidia watu walioathirika.

“Maporomoko ya ardhi yametokea katika eneo la Kimende Escarpments kaunti ya Kiambu. Watu kadhaa wanaaminika kuwa wamenaswa. Timu ya Msalaba Mwekundu iko njiani kuelekea eneo la tukio,” shirika hilo lilisema.

Haya yanajiri wiki chache tu baada ya takriban miili 40 kukusanywa kutoka maeneo mbalimbali baada ya mafuriko makubwa kusomba nyumba kadhaa katika Kijiji cha Kamuchiri Mai Mahiu, Kaunti ya Nakuru kufuatia mvua kubwa iliyonyesha.

Kamanda wa polisi wa Naivasha Stephen Kirui alithibitisha kuwa walikuwa wamekusanya takriban miili 40 kutoka kwa vifusi siku ya Jumatatu.

“Tuna miili 40 kufikia sasa iliyokusanywa na mingine mingi imefunikwa na tope. Magari mengi pia yamefunikwa,” alisema kutoka eneo la tukio.

Maafisa katika hifadhi hiyo ya maiti walisema wamepokea miili 42.

Vikosi vya uokoaji vilisema kuwa magari matano yalinaswa kwenye tope lakini miili ilikuwa imetolewa.

"Tunatarajia idadi hiyo kuongezeka wakati utafutaji na uokoaji unaendelea," afisa mmoja alisema.

Zaidi ya watu 100 walikimbizwa hospitalini kufuatia mkasa huo.

Wanyama wa nyumbani pia waliuawa katika tukio hilo, maafisa walisema.

Shughuli za uokoaji zilikuwa zikikwamishwa na utelezi wa eneo ambako maji yalitiririka.

Maji ya mafuriko yalitoka kwenye mto ulio karibu ambao ulivunja kingo zake, kulingana na Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya.