Ziara ya Rais Ruto Marekani: Kenya kuteuliwa kuwa mshirika mkuu asiyekuwa mwanachama wa NATO

Rais Biden alisema nchi hizo mbili zina wasiwasi sawa wa usalama kama vile kupigana na ISIS.

Muhtasari

•Biden alitangaza anashirikiana na Bunge kuteua Kenya kama mshirika mkuu asiyekuwa mwanachama wa Nato kuimarisha ushirikiano wa kiusalama.

•Rais Ruto alisema ushirikiano huo utainua mchango wa nchi yake katika uimarishaji wa amani katika Pembe ya Afrika.

Image: BBC

Rais wa Marekani Joe Biden alitangaza kuwa anashirikiana na Bunge kuteua Kenya kama mshirika mkuu asiyekuwa mwanachama wa Nato kuimarisha ushirikiano wa kiusalama.

Rais Biden alisema nchi hizo mbili zina wasiwasi sawa wa usalama kama vile kupigana na ISIS, msaada kwa Ukraine dhidi ya uvamizi wa Urusi na utulivu wa Haiti.

Biden alikuwa akizungumza katika Ikulu ya Marekani pamoja na Rais wa Kenya William Ruto ambaye yuko katika ziara ya kiserikali.

Rais Ruto alisema ushirikiano huo utainua mchango wa nchi yake katika uimarishaji wa amani katika Pembe ya Afrika.

Pia alisisitiza kujitolea kwa serikali yake kuongoza ujumbe wa Kimataifa wa Usaidizi wa Usalama nchini Haiti.

Kenya itakuwa taifa la kwanza la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara kuteuliwa kuwa mshirika mkuu asiyekuwa mwanachama wa Nato. Nchi nyingine za Afrika ni pamoja na Morocco, Misri na Tunisia.

Hadhi ya mshirika mkuu asiyekuwa mwanachama wa Nato huwapa washirika wa kigeni fursa ya mapendeleo ya kijeshi na kiuchumi na Marekani.