Polisi wa Kenya kuwasili Haiti katika kipindi cha 'wiki tatu'

Siku ya Ijumaa, wamishonari wawili wa Marekani waliuawa huko Haiti na magenge.

Muhtasari

•Ruto amesema polisi wanatarajiwa kuwasili Haiti kusaidia kuzima ghasia za magenge zinazoongezeka katika kipindi cha takribani wiki tatu.

•"Nina timu tayari Haiti ninapozungumza nawe," Bw Ruto aliiambia BBC Ijumaa.

Image: BBC

Rais wa Kenya William Ruto anasema jeshi lake la polisi wa kulinda amani linatarajiwa kuwasili Haiti kusaidia kuzima ghasia za magenge zinazoongezeka katika kipindi cha takribani wiki tatu.

Katika mahojiano ya kipekee na BBC, Bw. Ruto alithibitisha timu ilikuwa tayari Haiti na alikuwa amekutana na polisi wa eneo hilo ili kupata mipango kabla ya wanajeshi wa Kenya kutumwa.

Maoni ya Bw Ruto yalitolewa alipohitimisha safari ya siku tatu Washington DC, ikiwa ni ziara ya kwanza rasmi ya kiserikali nchini Marekani katika zaidi ya miaka 15.

Wakati wa safari yake, Ikulu ya Marekani ilitoa wito wa kutumwa haraka kwa kikosi cha kimataifa kinachoongozwa na Kenya, baada ya wanandoa wa Marekani kutajwa miongoni mwa wamishonari watatu waliouawa nchini Haiti siku ya Ijumaa.

"Nina timu tayari Haiti ninapozungumza nawe," Bw Ruto aliiambia BBC Ijumaa.

"Hiyo itatupa sura ya jinsi mambo yanavyoonekana ardhini, uwezo unaopatikana, miundombinu ambayo imewekwa."

Aliongeza: "Tunapopata tathmini hiyo tuliyokubaliana na polisi wa Haiti na uongozi wa Haiti, tunaangalia upeo wa kati ya wiki tatu na pale kuhusu sisi kuwa tayari kupeleka, mara kila kitu kitakapowekwa. "

Mwaka jana, Kenya ilijitolea kuongoza kikosi cha usalama cha kimataifa kinachoungwa mkono na Umoja wa Mataifa kurejesha utulivu katika kisiwa cha Caribbean.

Magenge yamechukua sehemu kubwa ya Haiti, na kuleta vurugu na uharibifu katika jiji lake kuu lililozingirwa, Port-au-Prince kufuatia mauaji ya Rais Jovenel Moïse mnamo Julai 2021.

Siku ya Ijumaa, wamishonari wawili wa Marekani waliuawa huko Haiti na magenge.

Bw Ruto aliambia BBC kwamba matukio ya aina hii ndiyo "hasa" sababu nchi yake ilikuwa inajiandaa kutuma jeshi lake la polisi.

"Hatupaswi kupoteza watu. Hatupaswi kuwa tunapoteza wamisionari," alisema.

"Tunafanya hivi ili kuzuia watu zaidi kupoteza maisha kwa magenge."

Marekani pia ni sehemu ya muungano wa mataifa mbalimbali unaofanya kazi na Kenya.

"Hali ya usalama nchini Haiti haiwezi kusubiri," alisema msemaji wa Baraza la Usalama la Kitaifa siku ya Ijumaa.

Walisema Rais Joe Biden aliahidi kuunga mkono "haraka ya kutumwa kwa jeshi" katika mazungumzo yake na Rais Ruto.

Bw Ruto alisema kuwa kambi ambapo wanajeshi na vifaa vitahifadhiwa, inayojengwa kwa ushirikiano na Marekani, inakaribia kwa "70% kukamilika".