NCIC: Kesi za matamshi ya chuki zimepungua

Alizungumza Jumatatu wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu hali ya amani na mshikamano nchini Kenya.

Muhtasari
  • Kobia alisema Tume ilipokea kesi 67 kati ya hizo 43 ziko katika hatua mbalimbali za upelelezi, mbili ziko mahakamani, 13 zimehitimishwa na nyingine 13 zilisuluhishwa kama vifungu vya Sheria ya NCI ya mwaka 2008.
Mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano Samuel Kobia
Image: NCIC/ X

Mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano Samuel Kobia amesema matamshi ya chuki na visa vya dharau za kikabila vimepungua.

Kobia alihusisha hili na ushirikiano unaoendelea na umma.

"Tume imeendelea kufuatilia kesi za matamshi ya chuki kwenye mitandao ya kijamii na majukwaa mengine ya umma," alisema

Kobia alisema Tume ilipokea kesi 67 kati ya hizo 43 ziko katika hatua mbalimbali za upelelezi, mbili ziko mahakamani, 13 zimehitimishwa na nyingine 13 zilisuluhishwa kama vifungu vya Sheria ya NCI ya mwaka 2008.

Alizungumza Jumatatu wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu hali ya amani na mshikamano nchini Kenya.

"Kuhusiana na majukwaa ya Mitandao ya Kijamii, Tume iliripoti kesi 44 za ubaguzi, 24 za uchochezi, sita za matamshi ya chuki, 93 za habari potofu, na 68 za upotoshaji - jumla ya kesi 268," alisema.

Akizungumzia suala la magenge ya uhalifu ya vijana waliojihami kwa silaha alibainisha kuwa tume hiyo imeshuhudia mauaji na mashambulizi ya makundi hayo.

"Wakati ni kweli kwamba hali hii ya kijamii ya vijana ni matokeo ya ukosefu wa ajira rasmi kujikusanya kwao na kujihusisha na vitendo vya uhalifu kunaleta tishio kwa kitambaa dhaifu cha mafungamano ya kijamii," alisema.

Ili kukabiliana na changamoto hiyo, Kobia alibainisha kuwa tume imeanzisha mpango wa Peace to the City Initiative ambao shughuli yake ya uzinduzi ni kuitisha Mkutano wa Vijana walio katika Mazingira Hatarishi huko Nairobi mwezi Julai.

Pia alipongeza jitihada za serikali za kufungua vituo zaidi vya ulinzi na usalama pamoja na kuimarisha operesheni ya kuwaondoa wahalifu hivyo kuwahudumia Wananchi.