Rais Ruto asalimu amri, akiri wengi hawataki mswada wa fedha 2024/25

"Nikisikiliza kwa makini watu wa Kenya ambao wamesema kwa sauti kubwa kwamba hawataki chochote kuhusiana na Mswada huu"

Muhtasari

• Baada ya hapo, anatarajiwa kumtaka kiongozi wa wengi Kimani Ichungwa'h kuondoa rasmi.

• Rais Ruto aliendelea kusema kuwa utawala wake umefanya kazi kwa bidii na kwa uthabiti ili bei ya bidhaa muhimu kama vile ‘unga’ kushuka kutoka Sh240 hadi Sh100.

RAIS WILLIAM RUTO
Image: TWITTER

Rais William Ruto amesalimu amri shinikizo za wananchi na kusema kuondoa kabisa Mswada wa Fedha wa 2024.

Rais alisema wananchi wamezungumza.

"Nikisikiliza kwa makini watu wa Kenya ambao wamesema kwa sauti kubwa kwamba hawataki chochote kuhusiana na Mswada huu wa Fedha wa 2024, ninakubali na kwa hivyo sitatia saini Mswada wa Fedha wa 2024 na baadaye utaondolewa," alisema.

Mswada ukishakuwa mbele ya Bunge, hauwezi kupita tu hadi utakapotolewa.

Hivyo rais anatarajiwa kuurejesha Bungeni, pamoja na maelezo ya kwanini hatausaini kuwa sheria.

Baada ya hapo, anatarajiwa kumtaka kiongozi wa wengi Kimani Ichungwa'h kuondoa rasmi.

Rais Ruto aliendelea kusema kuwa utawala wake umefanya kazi kwa bidii na kwa uthabiti ili bei ya bidhaa muhimu kama vile ‘unga’ kushuka kutoka Sh240 hadi Sh100.

Katika hotuba yake kwa taifa kwa njia ya televisheni kutoka Ikulu, Rais alisema kwa kila Sh100 serikali inakusanya ushuru, Sh61 hutumika kulipa deni la nchi.

“Tumelipa deni la Eurobond la Kenya ambalo lilikopwa mwaka wa 2014 la dola bilioni 2 ambazo zimekuwa zikining’inia shingoni. Tulilipa awamu ya mwisho ya $500 milioni wiki jana,” Ruto alisema.