Ulimwangusha Rais! Gachagua amkashifu bosi wa NIS Noordin Haji

Kulingana na Gachagua, hasira kali iliyopelekea Wakenya kulivamia Bunge ni ishara tosha ya kushindwa kwani vitendo hivyo havijawahi kushuhudiwa katika historia ya Kenya.

Muhtasari
  • DP alidai bosi wa NIS Noordin Haji alishindwa kumfahamisha Rais kuhusu ukubwa wa maandamano hayo kwa wakati ili kuepusha mauaji na vifo visivyokuwa vya kawaida.
Image: DPCS

Naibu Rais Rigathi Gachagua amekashifu Idara ya Kitaifa ya Ujasusi ambayo anadai ilishindwa kumjulisha Rais kwa wakati kuhusu maandamano makubwa yaliyoshuhudiwa Jumanne.

DP alidai bosi wa NIS Noordin Haji alishindwa kumfahamisha Rais kuhusu ukubwa wa maandamano hayo kwa wakati ili kuepusha mauaji na vifo visivyokuwa vya kawaida.

"Noordin Haji lazima awajibike kwa vifo, ghasia, kumwangusha Rais Ruto na Kenya kwa kutofanya kazi yake. Ni lazima afanye jambo la heshima, sio tu kuwajibika bali ajiuzulu," Gachagua alisema.

"NIS ililala kazini. Ilibidi watu wafe na maandamano kote nchini ili Ruto ajue ukweli kuhusu watu wa Kenya wanahisi ilhali kuna shirika limelipwa na umma ili kumjulisha rais kuhusu hisia za Wakenya," DP aliongeza.

Kulingana na Gachagua, hasira kali iliyopelekea Wakenya kulivamia Bunge ni ishara tosha ya kushindwa kwani vitendo hivyo havijawahi kushuhudiwa katika historia ya Kenya.

Naibu Rais pia aliendelea kusifu Gen Z kwa kutoa sauti zao.

"Ninataka kumwita Gen Z atuambie ni nani wa kuhusika kwa sababu hawana kabila, hawana kiongozi na hawana muundo wa shirika lakini tungependa kushirikiana na watu wanaofaa."