Mbunge wa Turkana ya Kati Joseph Namuar aomba radhi kwa kuunga mkono Mswada wa Fedha

"Na kama kuna njia ambayo tulikosea sisi ambao tulipiga ndiyo tunaomba msamaha," Namuar alisema.

Muhtasari

• Namuar alisema kuwa Ruto anakubali na kusikiliza semi za watu.

• Mnamo Jumatano, Ruto alitangaza kwamba hatatia saini Mswada wa Fedha wa 2024 ambao ulikuwa na utata mkubwa, na kuzua maandamano makubwa kote nchini.

Mbunge wa Turkana ya Kati Joseph Namuar Picha: HESBORN ETYANG
Mbunge wa Turkana ya Kati Joseph Namuar Picha: HESBORN ETYANG

Mbunge wa Turkana ya Kati Joseph Namuar wa chama cha UDA amewaomba wakazi wa eneo bunge lake msamaha baada ya kuunga mkono Mswada wa Fedha.

Katika video iliyoonekana na meza yetu ya habari, mbunge huyo pia alimpongeza Rais William Ruto kwa kutotia saini Mswada wa Fedha.

"Na kama kuna njia ambayo tulikosea sisi ambao tulipiga ndiyo tunaomba msamaha," Namuar alisema.

Namuar alisema kuwa Ruto anakubali na kusikiliza semi za watu.

"Nampongeza kwa sababu ya uongozi ambao amedhibitisha siku ya leo kuhakikisha kila mkenya ameweza kujua ya kwamba rais ni mtu wa kuskiza maoni yao," alisema.

(Naupongeza uongozi wa Rais Ruto katika kuhakikisha kuwa kila mtu wa kawaida anajua kuwa rais anasikiliza maoni yao).

Mnamo Jumatano, Ruto alitangaza kwamba hatatia saini Mswada wa Fedha wa 2024 ambao ulikuwa na utata mkubwa, na kuzua maandamano makubwa kote nchini.

"Baada ya kutafakari juu ya mazungumzo yanayoendelea kuhusu maudhui ya Mswada wa Fedha wa 2024, na kusikiliza kwa makini watu wa Kenya ambao wamesema kwa sauti kubwa kwamba hawataki chochote cha kufanya na Mswada huu wa Fedha wa 2024, nakubali, na kwa hivyo sitatia saini mswada wa fedha wa 2024," Ruto alisema katika hotuba yake kupitia televisheni.

Uamuzi huo wa Rais umekuja siku moja tu baada ya Mswada huo kupitishwa na Bunge, licha ya maandamano ya nchi nzima kuupinga.