Mama mkwe wa mshukiwa wa mauaji ya Kware azungumza, aeleza kwa nini hakuripoti kupotea kwa bintiye

Josephine sasa ameiomba serikali kumsaidia kupata haki kwa bintiye akisema ana uchungu mwingi moyoni.

Muhtasari

•Josephine alidai kuwa binti yake alitoroka nyumbani mwaka wa 2021 baada ya kukataa kuendelea na masomo yake.

•Alisema mshukiwa wa mauaji ya Kware hakujulikana katika familia yao kwani hawakujua kuwa ndiye alikuwa na binti yao.

Miili hiyo ilitolewa kwenye eneo la taka Kware, kaunti ya Nairobi mnamo Julai 12, 2024
Image: RADIO JAMBO

Bi Josephine Adisa, mwanamke anayeaminika kuwa mama ya mwanadada anayeripotiwa kuwa mke wa zamani wa mshukiwa mkuu wa mauaji ya Kware mnamo Jumatatu aliandikisha taarifa na wapelelezi wa DCI.

Josephine alisema Imelda, ambaye anadaiwa kuwa mwathirika wa kwanza wa mshukiwa wa mauaji ya Kware, ni mtoto wake wa pili.

Alidai kuwa binti yake alitoroka nyumbani mwaka wa 2021 baada ya kukataa kuendelea na masomo yake.

“Alipotea lakini wakati mwingine alikuwa kwa mtandao anachat na wengine. Lakini ilipofika 2022, akaunti yake ikanyamaza. Akiandikiwa ujumbe, hawezi kujibu. Tangu wakati huo sikumskia tena, ndio nimeskia ripoti kwamba aliuawa,” Bi Josephine alisema.

Aliweka wazi kuwa hakuwahi kuandikisha ripoti yoyote kuhusu kupotea kwa binti yake kwani mwanzoni alikuwa akipiga gumzo na watu kwenye mitandao ya kijamii.

“Sikuripoti kwa sababu alikuwa anaonekana kwa mitandao, alikuwa anachat na wengine. Sasa nikajua tu ako. Lakini vile ilifika 2022 nauliza dadake kama anaongea naye akaunti akaunti yake haifanyi. Nauliza dadake mkubwa, akaunti akaunti yake haifanyi. Nauliza kila wakati, wanasema hawamskii. Sasa leo ndio nimeshtukia ripoti kwamba ameuawa, nikapatwa na mshtuko,” alisema.

Alibainisha kuwa mshukiwa wa mauaji ya Kware hakujulikana katika familia yao kwani hawakujua kuwa ndiye alikuwa na binti yao.

Josephine sasa ameiomba serikali kumsaidia kupata haki kwa bintiye akisema ana uchungu mwingi moyoni kutokana na kile kilichompata.

“Watoto nilikuwa nimewalea na shida nyingi na nilikuwa na matarajio kwamba siku moja atanisaidia,” alisema.

Akiongea na wanahabari siku ya Jumatatu, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai Mohamed Amin alidai kuwa mwathiriwa wa kwanza wa mshukiwa wa mauaji ya Kware alikuwa mke wake.

"Mshukiwa alidai kuwa mwathiriwa wa kwanza alikuwa mke wake ambaye alimnyonga hadi kufa kabla ya kuukata na kuutupa mwili wake katika eneo la Kware," Amin alisema.