Paul Kagame ashinda urais wa Rwanda kwa zaidi ya 99% ya kura

Habineza alikuwa katika nafasi ya pili na asilimia 0.53 ya kura huku Mpayimana akipata 0.32%.

Muhtasari

•Matokeo ya awali ya uchaguzi yaliyotolewa Jumatatu jioni yalionyesha kuwa Kagame ameshinda kura kwa 99.15%.

•Wagombea wengine kadhaa, wakiwemo wakosoaji wengi wa Kagame, walizuiwa kuwania urais.

Rais wa Rwanda Paul Kagame
Image: BBC

Rais wa Rwanda Paul Kagame ameshinda tena uchaguzi wa urais wa nchi hiyo kwa zaidi ya asilimia 99 ya kura.

Matokeo ya awali ya uchaguzi yaliyotolewa Jumatatu jioni yalionyesha kuwa Kagame ameshinda kura kwa 99.15% ya 79% ya kura zilizohesabiwa hadi Jumatatu jioni.

Baraza la uchaguzi nchini humo lilisema kuwa jumla ya waliojitokeza kupiga kura ni 98% ya wapiga kura milioni 9 waliojiandikisha.

Kati ya 78.94% ya kura zilizohesabiwa kufikia mwendo wa saa mbili jioni, Kagame alikuwa mbele kwa 99.15% ya kura.

Kagame ambaye amekuwa madarakani katika nyadhifa mbalimbali tangu 1994, alishinda kwa kiasi sawa na hicho mwaka wa 2017.

Kagame alipiga kura yake karibu mchana katika kituo cha kupigia kura mjini Kigali. Alikuwa amesema kwamba vipaumbele vyake vya kujenga nchi kuelekea ustawi havitabadilika.

Kagame, ambaye alichaguliwa kuwa rais kwa mara ya kwanza mwaka 2000, alikabiliana na wagombea wengine wawili: Frank Habineza wa chama cha Democratic Green Party na Philippe Mpayimana ambaye ni mgombeaji huru.

Habineza alikuwa katika nafasi ya pili na asilimia 0.53 ya kura huku Mpayimana akipata 0.32%.

Hii ilikuwa ni jaribio la pili kwa Mpayimana, mwanahabari aliyegeuka kuwa mwanasiasa ambaye mipango yake ya kuendeleza kilimo, uchukuzi, uvuvi na viwanda vingine iliangaziwa katika makala 50 zaidi.

Habineza ambaye pia alishindana na Kagame katika uchaguzi uliopita alisema ameingia tena kwenye kinyang’anyiro hicho mwaka huu kwa sababu rais Kagame amekaa muda mrefu na ni wakati wa kuwa na dira mpya kwa nchi.

Wagombea wengine kadhaa, wakiwemo wakosoaji wengi wa Kagame, walizuiwa kuwania urais.

Takriban milioni 9 kati ya wakazi milioni 14 wa Rwanda walijiandikisha kupiga kura.