Nchi za Magharibi zatoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi kuhusu matukio ya upoteaji, ukatili na vifo nchini Tanzania

Zinataka mamlaka kuchukua jukumu la kulinda haki za msingi za wananchi ikiwa ni pamoja na uhuru wa kujieleza.

Muhtasari

• Mabalozi wa nchi za magharibi  walihimiza serikali ya Tanzania kuhakikisha ulinzi wa upinzani kama alivyoahidi Rais waTanzania Dr samia Suluhu kupitia mpango wake wa ’’4R.

aliagiza uchunguzi ufanyike kufuatia mauaji ya hivi karibuni ya mwanasiasa wa upinzani
Rais Samia Suluhu Hassan aliagiza uchunguzi ufanyike kufuatia mauaji ya hivi karibuni ya mwanasiasa wa upinzani

Mabalozi wa Umoja wa Ulaya, Ubalozi wa Uingereza, Canada, Norway na Uswisi nchini Tanzania, wameeleza kusikitishwa na vitendo vya hivi karibuni vya ukatili, kupotea kwa watu na vifo vya wanahakati wa kisiasa na haki za binadamu.

Katika tamko la pamoja lililotumwa kwenye mitandao ya kijami, mabalozi hao wamesema: ‘‘Tunatoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi wa kina kuhusu matukio haya’’.

Tunaihimiza serikali ya Tanzania kuhakikisha ulinzi wa upinzani kama alivyoahidi Rais waTanzania Dr samia Suluhu kupitia mpango wake wa ’’4R’’, na mamlaka kuchukua jukumu la kulinda haki za msingi za wananchi ikiwa ni pamoja na uhuru wa kujieleza’’, tamko la mabalozi hao limeeleza.

Tamko hilo la mabalozi wa Magharibi nchini Tanzania linajiri baada ya Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan wiki iliyopita kuagiza uchunguzi baada ya kifo cha Kiongozi wa chama cha Upinzani Tanzania Chadema Ally Mohamed Kibao aliyetekwa kisha kuuawa, kulingana na Polisi nchini humo.

"Nimeagiza vyombo vya uchunguzi kuniletea taarifa ya kina kuhusu tukio hili baya kabisa na mengine ya namna hii haraka. Nchi yetu ni ya kidemokrasia na kila raia ana haki ya kuishi. Serikali ninayoiongoza haivumilii vitendo vya kikatili vya namna hii,"anaandika katika ukurasa wake wa X.

Katika Tamko lao mabalozi hao wamepongeza hatua ya Rais Samia ya kutoa wito wa uchunguzi dhidi ya matukio ya hivi karibuni: ‘’Tunakaribisha wito wa rais wa kuanzisha uchunguzi wa haraka ili kubaini wahalifu waliohusika na kuhakikisha kunakuwa na uwajibikaji’’, lilisema tamko hilo.

'' Tunatambua kwamba matukio haya yanatishia demokrasia na haki za wananchi wa Tanzania , katika nchi inayoheshimika kwa amani na utulivu na tunaungana na wito wa kulinda amani na utulivu wa nchi'', tamko hilo lilihitimisha.