Shughuli zavurugwa JKIA Jumanne usiku, wafankayazi wa KAA wagoma

Wafanyakazi wameapa kuvuruga shughuli za kawaida hadi pale serikali itakapositisha mkataba wake na Adani.

Muhtasari

• Mgomo huo ulisababisha ratiba za safari za ndege kuvurugika, huku abiria wengi wakikwama kwenye uwanja wa ndege.

Ndege katika uwanja wa JKIA
Ndege katika uwanja wa JKIA
Image: DOUGLAS OKIDDY

Misururu mirefu ilishuhudiwa Jumanne usiku katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) huku wafanyikazi wa anga wakianza mgomo.

Mgomo huo unafuatia notisi iliyotolewa na Chama cha Wafanyakazi wa Usafiri wa Anga (KAWU) mnamo Agosti 12, 2024, ambapo walipinga pendekezo la kukodisha uwanja wa ndge wa kimataifa JKIA kwa kampuni ya Adani kutoka India.

Katibu Mkuu wa KAWU Moss Ndiema, akitoka notisi ya mgomo, alisema kuwa mkataba wa JKIA-Adani ungesababisha kupunguzwa kwa wafanyakazi wengi, kuajiriwa kwa wafanyikazi wa kigeni, pamoja na mazingira duni ya kazi.

Wafanyakazi hao walitaka Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (KAA) na mameneja watatu wakuu kujiuzulu, wakiwashutumu kwa uzembe na kushughulikia vibaya mpango huo.

Aidha walitaka mameneja wawili wa usalama wa shirika la ndege la Kenya Airways kujiuzulu wakitaja utovu wa nidhamu, ikiwa ni pamoja na shutuma za ulanguzi wa binadamu, unyanyasaji wa kijinsia, na kupandishwa vyeo kwa njia isiyo ya haki ndani ya idara hiyo.

Mgomo huo siku ya Jumanne usiku ulisababisha ratiba za safari za ndege kuvurugika, huku abiria wengi wakikwama kwenye uwanja wa ndege.

Wafanyakazi hao wameapa kuvuruga shughuli za kawaida hadi pale serikali itakapositisha mkataba wake na Adani.