Vikao vya Bunge kurejelewa Jumanne, September 17

Hii ni baada ya mapumziko marefu ya wabunge na kufanyia wananchi kazi katika maeneo bunge yao.

Muhtasari

• Bunge linarejelea vikao vyake baada ya mapumziko marefu ya wabunge kuendeleza miradi katika maeneo bunge yao.

• Uchambuzi wa ripoti ya kamati kuhusu uteuzi wa Bw. Douglas Kanja kuongoza NPS kupewa kipaombele.

Bunge la Kenya
Wabunge wa Kenya wakiwa kikaoni Bunge la Kenya
Image: Twitter @NAssembly Kenya

Bunge la kitaifa limerejelea vikao vyake vya sehemu ya tatu katika kikao cha tatu tarehe 17 Septemba baada ya mapumziko ya muda mrefu.

Wabunge wanarudi vikaoni kujadili miswada miseto pamoja na kuangazia ripoti za kamati zilizobuniwa kupiga msasa wateuzi watakaosimamia bodi na idara mbali mbali za serikali.

Ajenda kuu itakayojadiliwa na watunzi hao wa sheria ni kuangazia ripoti ya kamati ya pamoja ya bunge iliyompiga msasa inspekta jenerali wa polisi mteule Bw. Douglas Kanja.

Bwana  Kanja aliteuliwa na rais Dkt. William Ruto kuchukua uongozi wa huduma za kitaifa ya polisi baada ya Japheth Koome kujiuzulu kufuatia maandamano ya kupinga mswada wa fedha ya mwaka 2024/25 yaliyofanywa Gen Z.

Wabunge pia wataangazia ripoti ya kamati ya pamoja ya bunge ya uteuzi wa mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya ushindani.

Aidha mswada wa kahawa ya mwaka 2023, mswada wa Sheria ya Mfuko wa Usawazishaji (Utawala) (2023) na mswada Mung Beans ya mwaka 2022 itasomwa kwa mara ya pili kwenye vikao hivyo vya awamu ya tatu.

Mswada wa kahawa 2023 unalenga kudhibiti tasnia ya kahawa, kuhakikisha biashara ya haki na maendeleo endelevu.

Bunge litazingatia Mswada wa Ugavi wa Ziada wa Serikali za Kaunti (2024). Mswada huo ambayo unalenga kuweka masharti ya kuhamisha mgao wa masharti na usio na masharti kutoka kwenye sehemu ya mapato ya serikali ya kitaifa na kutoka kwa washirika wa maendeleo hadi serikali za kaunti kwa Mwaka wa Fedha wa 2024/25.

Aidha katika vikao vya bunge vya awamu ya tatu, bunge pia litaangalia wateule mbali mbali wa tume chini ya sheria ikiwemo tume ya mishahara na marupurupu(SRC), tume ya kitaifa ya jinsia na usawa na tume ya haki ya utawala.