DCI yapendekeza Mkurugenzi wa First Choice kufunguliwa mashtaka

Waathiriwa 201 wameandikisha taarifa na idara ya polisi ya DCI jinsi walivyolaghaiwa maelfu ya pesa na kampuni hiyo

Muhtasari

• Mkurugenzi wa First Choice anadaiwa kuwalaghai wakaazi wa Eldoret mamilioni ya fedha kwa kuwaahidi kazi katika mataifa ya kigeni.

• DCI imependekeza ofisi ya DPP kumfungulia mashtaka baada ya waathiriwa 201 kuandikisha taarifa ya idara hiyo.

Akiwa mbele ya kamati ya leba ya seneti Agosti 30, 2023
Mkurugenzi wa First Choice Judy Chepchirchir Akiwa mbele ya kamati ya leba ya seneti Agosti 30, 2023
Image: EZEKIEL AMING'A

Ofisi ya mkurugenzi wa upepelezi wa makosa ya jinai DCI imependekeza kufunguliwa kwa mashataka dhidi ya Judy Chepchirchir.

Chepchirchir ambaye ni mkurugenzi wa First Choice Recruitment and Consultancy Agency anadaiwa kupokea fedha kutoka kwa wananchi kupitia njia za udanganyifu.

Msaidizi wa Inspekta Jenerali wa DCI Paul Wachira akiwa mbele ya kamati ya kazi na ustawi wa jamii katika bunge la seneti mnamo Septemba 17 alielezea kamati hiyo kuwa takribani waathiriwa 201 wa udanganyifu kupitia kampuni ya Judy Chepchirchir wamerekodi taarifa.

Aidha bw. Wachira amesema kuwa idadi kamili ya waathiriwa huenda ni zaidi ya wale 201 walioandikisha taarifa na DCI.

Hata hivyo, Bw. Wachira amesema kuwa faili ya uchunguzi imerejeshwa kwa ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma DPP ikiitaka ofisi hiyo kumfungulia mashtaka Judy Chepchirchir.

Kampuni ya First Choice Recruitment and Consultancy inadaiwa kuwalaghai wakaazi wa kaunti ya Uasin Gishu zaidi ya shilingi bilioni moja kwa kuwahada kwamba wangalipata nafasi za ajira katika mataifa ya kigeni kama vile Qatar, Canada, Australia, Poland na Saudi Arabia.

Awali mwaka jana mwezi Agosti, Chepchirchir alisema kuwa aliwarejeshea waathiriwa 448 hela zao baada ya kukosa kupata nafasi za ajira kama alivyokuwa amewaahidi.

Aidha kamati ya kazi na ustawi wa jamii ya seneti baada ya kusikia mapendekezo ya DCI,imependekeza kampuni ya First Choice Recruitment and Consultancy Agency kufungwa kwa angalau miaka mitano.