Itumbi apuuzilia mbali madai ya DP Gachagua kuondolewa kwa WhatsApp ya rais

Gachagua aliongeza kuwa kama hayupo katika shughuli yoyote ya rais, ni kwa sababu kutofahamu uwepo wa hafla hiyo.

Muhtasari

• Gachagua alidai ukuwepo hila katika madhumuni ya yule alimuondoa katika ratiba ya rais ili aonekane mtovu. 

Image: FACEBOOK// DENNIS ITUMBI

Mkuu wa Uchumi bunifu na Miradi Maalum katika Afisi ya Rais Dennis Itumbi amemjibu Naibu Rais Rigathi Gachagua kwamba aliondolewa kwenye kikundi cha WhatsApp cha ratiba ya Rais William Ruto. 

Kulingana na Itumbi, Ruto alikuwa mtu wa kwanza kuondolewa kwenye kundi hilo la WhatsApp.Aliendelea kusema kuwa kundi hilo lilifutwa baada ya nyaraka za kisiri katika kundi hilo kuanza kutolewa nje ya kundi hilo hadi makundi mengine. 

"Ndio, kundi la Diary lilifutwa. Kile ambacho DP @rigathi anashindwa kutaja ni kwamba Rais aliondolewa hata kabla yake, na Kundi hilo lilifutwa kabisa kutokana na nyaraka zilizoainishwa sana kushirikiwa katika vikundi vingine vya WhatsApp," Itumbi alisema. 

Matamshi yake yalijiri baada ya Gachagua kulalamikia kuondolewa kwake kutoka kundi hilo na baadhi ya wahudumu wa rais. Naibu rais alisema kuondolewa kwa kundi hilo la WhatsApp kulifanya iwe vigumu kwake kujua ratiba za rais William Ruto. 

Alitaja kukosa matukio muhimu ya urais kutokana na ukosefu wa habari kuyahusu. Gachagua aliongeza kuwa kama hayupo katika shughuli yoyote ya rais, ni kwa sababu kutofahamu uwepo wa hafla hiyo.  Hata hivyo, alisema kuwa atapata muda mwafaka wa kuzungumza na rais na kutatua suala hilo.

"Siku zote huwa nalinganisha ratiba yangu na ile ya Rais, kila mara, na najipanga ipasavyo. Wakati mwingine nisipofahamu, nashindwa kuoanisha kwa sababu pia ninayo mipango yangu," alisema wakati wa mahojiano na Citizen TV.

Naibu rais alisema kwamba kila anapofahamu programu za Ruto, yeye hujitokeza kila mara. Gachagua alidai ukuwepo hila katika madhumuni ya yule alimuondoa katika ratiba ya rais ili aonekane mtovu. 

"Wakati mwingine wanataka nichelewe ili ionekane sina heshima, nataka niwaombe watu wanaofanya kazi za urais wasilete mgogoro kati yangu na Rais, mimi ni Naibu Rais wa Jamhuri ya Kenya niliyechaguliwa na wananchi, na Msaidizi Mkuu," DP aliongeza.