Ajuza wa miaka 71 adaiwa kuuawa na mwanawe baada ya kukataa kuuza shamba

Abuya anadaiwa kuwalipa wauaji ili wamuue mama yake Yunis Bitengo

Muhtasari

•Abuya anadaiwa kuwalipa wauaji wamuue mama baada kukataa ombi lake la kukata sehemu ya shamba kwa ajili ya kuuzwa.

•Kiungo cha mwili wa marehemu kilipatikana ndani ya shamba la mahindi, kilomita moja kutoka nyumbani kwake.

nyumbani kwa Yunis Bitengo 71, huko Nyakeyo, Mugirango Kusini, ambaye alichinjwa kwa sababu ya mkataba wa uuzaji wa ardhi ulioharibika.
Waombolezaji waliofadhaika nyumbani kwa Yunis Bitengo 71, huko Nyakeyo, Mugirango Kusini, ambaye alichinjwa kwa sababu ya mkataba wa uuzaji wa ardhi ulioharibika.
Image: MAGATI OBEBO

Polisi katika kaunti ya Kisii wanawazuilia washukiwa kumi kuhusiana na madai ya utekaji nyara na mauaji ya nyanya wa umri wa miaka 71 kutokana na dili ya uuzaji wa shamba iliyoharibika.

Miongoni mwa waliokamatwa Jumanne kama washukiwa ni pamoja na mwanawe marehemu- Moses Abuya- ambaye alihutubia wanahabari nyumbani siku ya Alhamisi.

Abuya anadaiwa kuwalipa wauaji ili wamuue mama yake Yunis Bitengo, ambaye ni mjane, baada ya kukataa kuitikia ombi lake la kukata sehemu ya shamba ya familia kwa ajili ya kuuzwa.

Wengine wanaozuilia ni mwanamke mmoja anayesemekana kuwa mzee wa kijiji, vijana wengine watatu na wazee watano.

Washukiwa hao walikamatwa baada ya barua ya kukiri makosa iliyoandikwa kwa mkono ikiorodhesha majina yao kupatikana kando ya njia.

Kulingana na barua hiyo, mwanawe marehemu anasemekana kulipa Sh4000 kama amana ya awali ya mauaji ya mamake.

Alipaswa kulipa Sh2000 za ziada baada ya kukamilika kwa mpango huo.

Wanakijiji walipata mkono na skafu ya marehemu wakati wa upekuzi huku mwili wake ukiwa haujapatikana wiki nne baada ya tukio hilo.

Kiungo cha mwili wake kilipatikana ndani ya shamba la mahindi, kilomita moja kutoka nyumbani kwake katika kijiji cha Getonto huko Nyakeyo.

Siku ya Jumanne, wapelelezi walisema bado wanafuatilia miongozo muhimu ambayo huenda ikasababisha kukamatwa kwa washukiwa wengine kadhaa.

"Bado tunafuata vidokezo muhimu ambavyo vinaweza kusababisha kukamatwa kwa washukiwa waliosalia; ni suala la siku chache," mmoja wa maafisa wanaoendesha uchunguzi wa tukio hilo alisema.

Bitengo alikuwa akinywa pombe katika nyumba moja kijijini hapo kabla ya kukokotwa usiku na kuuawa.

Polisi walisema washukiwa ambao tayari wamekamatwa bado hawajafichua sehemu ziingine za mwili zilipo.

"Hakuna jiwe litakaloachwa, kila mshukiwa anayehusishwa na mauaji yake na kutoweka kwa mwili baadae wote watafikishwa mahakamani," afisa huyo ambaye hakutaka kufichua utambulisho wake kwa kuhofia kuathiri uchunguzi.

Washukiwa hao watafikishwa mahakamani wiki hii.