DP Gachagua avunja kimya kuhusu matamshi ya Ruto ya kuwa na mgombea mwenza mwanamke

Rais Ruto aliahidi kuhakikisha kuwa chama chake cha UDA kitakuwa na naibu wa rais mwanamke katika siku za usoni.

Muhtasari

•Akizungumza katika kaunti ya Embu siku ya Ijumaa, Gachagua  alibainisha kuwa matamshi ya Rais Ruto hayakueleweka pakubwa.

•Rigathi alibainisha rais ana nia njema kwa wanawake akisema amekuwa akitaka wanawake kujumuishwa katika uteuzi serikalini.

Rais William Ruto na Naibu wake Rigathi Gachagua
Image: ANDREW KASUKU

Naibu Rais Rigathi Gachagua ametoa maoni yake kuhusu matamshi ya hivi majuzi ya Rais William Ruto akipendekeza kuwa katika siku zijazo, wagombeaji wowote wa UDA wa kiume watalazimika kuwa na mwanamke kama mgombea mwenza.

Akizungumza katika kaunti ya Embu siku ya Ijumaa, kiongozi huyo taifa wa pili  alibainisha kuwa matamshi ya Rais Ruto Alhamisi hayakueleweka pakubwa.

Alibainisha kuwa watu wengi walidhani kuwa rais alikuwa anazungumzia mipango ya mara moja ilhali kwa mujibu wake, wanapanga kutekeleza mpango huo baada ya kumaliza mihula yao.

“Na vile rais ulisema jana, ni kweli tumeongea na tutaendelea kuongea vile akina mama huko mbele watashirikishwa katika serikali kuu wakiwa na nyadhifa ambazo ziko na uzito. Kwa sababu hawa akina mama wamejionyesha kwamba wako na umaarufu na wanaweza kupewa nafasi ya kuongoza. Hiyo tumekubaliana,” DP Rigathi Gachagua alisema.

Aliongeza, “Lakini wengine hawakuelewa. Rais alisema ataniongelesha, tuwapange pale mbele tukimaliza mambo yetu. Sasa wengine walikuwa wanafikiria ni saa hii. Lazima mngoje kwanza nimsaidie rais kwa kipindi chake, ikifika kutamatisha hapo, rais mwenyewe atatuongoza. Atatuonyesha vile tutapanga hawa kina mama na vile mambo yao yatakuwa sawasawa.”

Rigathi alibainisha kuwa rais ana nia njema kwa wanawake wa Kenya akisema kuwa amekuwa akitaka wanawake kujumuishwa katika uteuzi serikalini.

Siku ya Alhamisi, Rais William Ruto aliahidi kuhakikisha kwamba chama chake cha UDA kitakuwa na naibu wa rais mwanamke katika siku za usoni.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa hafla ya Mkakati wa Baraza la Magavana wa G7 wa Baraza la Magavana katika Safari Park, Ruto alisema ataketi na naibu wake Rigathi Gachagua na kukubaliana kwamba ikiwa chama kitakuwa na mwanamume, mgombea mwenza lazima awe mwanamke.

Rais alisema hii itahakikisha chama chake kinaongoza kutoka mbele katika kuunga mkono wanawake na hivyo kusaidia katika kufikia sheria ya kijinsia ya thuluthi mbili.

"'Mimi na Riggy G baadaye tunapojadili siasa zetu zijazo lazima pia tukubaliane kwamba kwenda mbele kama mwanamume ni mgombea wa Urais katika chama chetu mwanamke lazima awe mgombea mwenza na ikiwa mwanamke ni mgombea basi mwanamume anaweza. kuwa mgombea mwenza,” rais alisema.

"Tutafanya hivi sio kwa sababu tunataka kufanya chochote dhidi ya wanaume lakini kwa sababu tunataka kusawazisha ili sote tusonge pamoja."

Rais alisema sheria hiyo hiyo itatolewa kwa kaunti ambapo wagombea wa ugavana wanaume watahitajika kuwa na wagombea wenzi wa kike na kinyume chake.