Fuliza yapunguza ada ya kila siku ili kuwavutia watumizi zaidi

Ada mpya itaanza kutumika tarehe 1 Oktoba 2022.

Muhtasari

•Kulingana na kampuni ya Safaricom,  hatua hiyo itasaidia ukuaji wa matumizi ya huduma za mkopo.

•Wakopaji wa kati ya Sh101 hadi Sh500 watatozwa ada ya kila siku ya Sh3, chini kutoka Sh5.

Afisa mkuu mtendaji wa Safaricom Peter Ndegwa akizindua programu ya M-Pesa mnamo Juni 23, 2021.
Afisa mkuu mtendaji wa Safaricom Peter Ndegwa akizindua programu ya M-Pesa mnamo Juni 23, 2021.
Image: SAFARICOM

Huduma ya mkopo ya Fuliza imepunguza ada zake za kila siku kwenye mkopo kwa asilimia 40.

Siku ya Jumatano huduma ya Safaricom na benki za NCBA na KCB zilitangaza punguzo ya ada, ambayo kulingana na kampuni hizo ni hatua ambayo itasaidia ukuaji wa matumizi ya huduma za mkopo.

"Tumeendelea kutathmini mabadiliko ya tabia ya watumiaji na hali ya kiuchumi ili kutambua njia ambazo tunaweza kuboresha zaidi matumizi ya huduma zetu za kifedha za kidijitali," Fuliza alisema katika taarifa yake.

"Kufikia hilo, tunaleta punguzo jipya la ada la hadi 40% kwa Fuliza."

Katika mabadiliko hayo, wakopaji wa kati ya Sh101 hadi Sh500 watatozwa ada ya kila siku ya Sh3, chini kutoka Sh5.

Mkopo woyote iliyozidi Sh501 hadi Sh1,000 itavutia ada ya kila siku ya Sh6 chini kutoka Sh10.

Ada mpya itaanza kutumika tarehe 1 Oktoba 2022.

Fuliza alitangaza zaidi kwamba mkopo wa chini ya Sh1,000 utakuwa na msamaha wa siku tatu kwa ada ya kila siku.