Masuala 5 muhimu ambayo Maaskofu wa Katoliki wanataka Rais Ruto ashughulikie

Kuhusu ukosefu wa ajira, maaskofu hao katika taarifa yao walibainisha kuwa vijana wengi hawana kazi.

Muhtasari

•Maaskofu hao walieleza kuwa gharama ya juu ya maisha imeathiri pakubwa na kutikisa mfumo wa kijamii wa jamii ya Kenya

Maaskofu wa katoliki
Maaskofu wa katoliki

Viongozi wa dini wamejitokeza kuiomba serikali kushughulikia masuala mbalimbali ili kufanya maisha ya wananchi wa kawaida kuwa bora.

Ijumaa, Baraza la Maaskofu wa katoliki nchiniKenya liliwasilisha suala  tano muhimu ambazo wanataka utawala unaoongozwa na Rais William Ruto kushughulikia mara moja.

Matano hayo ni pamoja na ushuru kupita kiasi, changamoto katika mfumo wa elimu, gharama ya juu ya maisha, kulinda utu wa watu wa Kenya na ukosefu wa ajira.

Kuhusu ukosefu wa ajira, maaskofu   hao katika taarifa yao  walibainisha kuwa vijana wengi hawana kazi.

"Tunakemea ufisadi ulio wazi ndani ya sekta ya umma, ambapo ukabila na ubaguzi unaonekana kuelekeza nafasi za kuajiriwa," inasomeka taarifa hiyo.

Kutokana na hali hiyo, Maaskofu waliliomba serikali kuwa na utaratibu wa uwazi na haki wa ajira hasa katika ofisi za umma.

Gharama kubwa ya maisha pia ilitajwa kuwa suala la kipaumbele ambalo linapaswa kuangaliwa.

Maaskofu hao walieleza kuwa gharama ya juu ya maisha imeathiri pakubwa na kutikisa mfumo wa kijamii wa jamii ya Kenya.

"Familia ziko katika mfadhaiko mkubwa wanapotatizika kupata riziki, na hivyo kusababisha uhusiano mbaya na kuongezeka kwa mivutano ndani ya kaya," walisema.

"Wazazi wanaona kuwa ni changamoto kutoa elimu ya Watoto wao, huduma ya afya na ustawi wa jumla," inasoma taarifa hiyo zaidi.

Maaskofu waliitaka serikali kufanya mashauriano na majadiliano mapana kati yao na wadau wengine, kupitia upya na kujifunza njia tunazoweza kushughulikia na kupunguza gharama kubwa za maisha.

Maaskofu hao walisema zaidi kwamba kwa kadiri mizozo katika Mashariki ya Kati ilivyoathiri gharama ya mafuta ya petroli, serikali inapaswa kujiepusha na kutoza ushuru kupita kiasi kwa Wakenya.

"Tunafahamu kuwa sehemu ya sababu ya kupanda kwa gharama ya maisha, kumetokana na mambo ya nje kama vile gharama ya mafuta ya petroli, na athari za migogoro ya Ukrania na Mashariki ya Kati," Maaskofu walisema.

Maaskofu wa Kikatoliki walitoa wito kwa serikali ya Kenya Kwanza kutafuta uwiano kati ya mapato yanayotakikana kwa serikali na ulinzi wa chini kabisa wa mahitaji ya kimsingi ya Mkenya wa kawaida kabisa, na heshima kwa utu wao.