Mhubiri Ezekiel Odero azuiwa kufanya krusedi nchini Tanzania, sababu 4 zatajwa

Mkutano huo ulitarajiwa kuanza Jumapili, Julai 16 hadi Julai 18.

Muhtasari

•Uongozi wa Jiji la Arusha ulifutilia mbali mkutano wa mhubiri wa Kenya Ezekiel Odero katika uwanja wa shule ya msingi ya Ngarenaro.

•Bw Juma alitaja kuwa Odero amehusishwa na tuhuma za vifo vya waumini na hivyo kumkaribisha huenda kungesababisha sintofahamu

Mchungaji Ezekiel Odero.
Mchungaji Ezekiel Odero.
Image: MAKTABA

Siku ya Jumapili, Uongozi wa Jiji la Arusha nchini Tanzania ulifutilia mbali mkutano wa mhubiri wa Kenya Ezekiel Odero katika uwanja wa shule ya msingi ya Ngarenaro.

Mhubiri huyo wa New Life Church alitarajiwa kuhubiria wafuasi wake nchini humo katika mkutano wa ‘Siku tatu za kubadilishwa na Mungu’ akishirikiana na Soni Nabii wa Tanzania. Mkutano huo ulitarajiwa kuanza Jumapili, Julai 16 hadi Julai 18.

Ripoti kutoka nchi hiyo jirani zinaarifu kwamba uongozi wa jiji la Arusha ulifutilia mbali mkutano huo kwa kile walichosema mhubiri huyo wa Kenya anahusishwa na madai ya mauaji ya waumini.

Gazeti la Mwananchi limeripoti kuwa kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Arusha ilisitisha kibali cha mkutano huo Jumapili asubuhi wakati mamia ya waumini wakiendelea na maombi. Maafisa wa usalama waliofika kwenye eneo la mkutano waliwaondoa waumini wale wakiwataka kutawanyika.

Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Juma Hamsini alisema kibali kilisitishwa baada ya utaratibu kutofuatwa. Alisema alipaswa kupelekewa barua ya maombi ya uwanja ili apate kujadiliana na maofisa wengine wa serikali kabla ya kibali kutolewa.

Pia alitaja kuwa Odero amehusishwa na tuhuma za vifo vya waumini na hivyo kumkaribisha huenda kungesababisha sintofahamu

Sababu nyingine ya kusitishwa kwa kibali cha mkutano huo ni kuwa eneo alilopewa Odero kuwahubiria waumini ni la shule na wanafunzi walikuwa katika kipindi cha mitihani.

Bw Juma pia aliibua wasiwasi kuhusu hofu ya kusambaa kwa ugonjwa wa matumbo ambao umezuka katika baadhi ya maeneo ya jiji hilo.

Mhubiri Ezekiel Odero amekuwa nchini Tanzania kwa siku kadhaa zilizopita katika ziara ya kuwahubiria na kuwaponya waumini katika taifa hilo la Afrika Mashariki.