Mlinzi wa kanisa la Kangemi adaiwa kutoweka na mchango wa milioni 1.5 uliotolewa Jumapili

Waumini walishangaa sana ni jinsi gani mlinzi huyo wa parokia aliyeaminiwa angefanya kitendo hicho kisichofaa.

Muhtasari

•Pesa ambazo waumini walikusanya Jumapili kwa ajili ya maendeleo ya kanisa  zilitoweka kwenye droo ya madhabahu ya Kanisa hilo.

•Mshukiwa anadaiwa kuvuruga nguvu za umeme za kanisa hilo kuzima mtambo wa CCTV uliowekwa kabla ya kutoweka na michango ya waumini.

Picha ya Kanisa
Picha ya Kanisa
Image: BIBLE STUDY TOOLS

Maafisa wa upelelezi katika kituo cha polisi cha Kangemi, kaunti ndogo ya Dagoretti, wameanzisha msako wa kumsaka mshukiwa anayedaiwa kuvunja kanisa na kuiba zaidi ya Shilingi milioni 1.5.

Katika tukio la kushangaza ambalo limewaacha makasisi na waumini wa Kanisa la ACK All Saints Mountain View huko Kangemi katika hali ya sintofahamu, pesa walizokusanya Jumapili kwa ajili ya maendeleo ya kanisa hilo zilitoweka kwenye droo ya madhabahu ya Kanisa hilo.

Mzee wa kanisa John Wainanina na mweka hazina Elizabeth Njoki, walipoenda kanisani kuchukua pesa Jumatatu asubuhi, walipata milango ikiwa wazi, jambo ambalo halikuwa la kawaida.

Kuitazama kwa makini meza ambapo mkate na divai hutolewa, walishangaa kuona ikiwa imevunjwa na pesa zilizokuwa zimehifadhiwa kwenye droo ya chini ya madhabahu hazipo!

Waliripoti kisa hicho mara moja katika kituo cha polisi cha Kangemi na katika uchunguzi wa awali, ilishukiwa kuwa mlinzi wa kanisa hilo George Mburu, anayeaminika kutoweka, alidaiwa kuhusika na wizi huo.

Anashukiwa kuvuruga nguvu za umeme za kanisa hilo kuzima mtambo wa CCTV uliowekwa kabla ya kutoweka na michango ya waumini.

Washiriki wa kanisa hilo ambao wanaishi karibu walioonekana kushtuka walikusanyika huku na huko wakizungumza kwa sauti ya chini, huku wakijaribu kuamini kutoweka kwa pesa zilizokusudiwa kwa maendeleo ya kanisa la jamii.

Walishangaa sana ni jinsi gani mlinzi huyo wa parokia aliyeaminiwa angefanya kitendo hicho kisichofaa.

Wengine walisikika wakitoa laana kwa mshukiwa ambaye walitangaza kwamba hatafanikiwa kamwe “katika kubaki kwake chini ya jua,” huku wengine wakimuombea msamaha iwapo angeibuka tena na kutubu dhambi zake.

Wakati huo huo, wapelelezi wameanzisha msako wa kumsaka mshukiwa ambaye alikuwa akiishi ndani ya boma la kanisa hilo, lakini mara moja akajificha kufuatia tukio hilo.