Mshtuko! Mzee apatikana amekufa katika loji Siaya, dawa za UKIMWI zapatikana kando ya mwili wake

Takriban tembe 90 za UKIMWI zilipatikana kando ya mwili wa marehemu,

Muhtasari

•Mwili wa mzee wa miaka 61 ulipatikana ndani ya chumba katika moja ya nyumba za wageni mjini Bondo.

•Marehemu hakuwa ameandamana na yeyote na alionekana amelewa kiasi, kulingana na ripoti ya polisi.

Rip
Rip
Image: HISANI

Mshtuko mkubwa ulikumba mji wa Bondo katika Kaunti ya Siaya siku ya Jumanne asubuhi baada ya mwili wa mzee wa miaka 61 kupatikana ndani ya chumba katika moja ya nyumba za wageni mjini humo.

Inaripotiwa kuwa mmoja wa wahudumu wa nyumba hiyo ya wageni aliupata mwili wa marehemu Nicholas Ogada Ogol ukiwa umelala juu ya kitanda wakati alipokuwa akitekeleza majukumu yake katika nyumba hiyo ya wageni siku ya Jumanne.

Mara moja msimamizi wa nyumba hiyo ya kulala wageni aliripoti tukio hilo la kutatanisha katika Kituo cha Polisi cha Bondo.

Maafisa wa polisi waliofika katika eneo la tukio walibaini kuwa marehemu aliingia katika nyumba hiyo ya wageni siku ya Jumatatu jioni. Hakuwa ameandamana na yeyote wakati huo na alionekana amelewa kiasi, kulingana na ripoti ya polisi.

Hali ya marehemu haikujulikana hadi siku ya Jumanne asubuhi ambapo mmoja wa wahudumu aliyekuwa akifanya usafi alipogundua mwili wake ukiwa umelala kitandani. Hakukuwa na majeraha yoyote yaliyoonekana kwenye mwili wa marehemu.

Takriban tembe 90 za dawa za matibabu ya ugonjwa wa UKIMWI zilipatikana kando ya mwili wa marehemu, mkuu wa polisi kaunti ya Siaya Cleti Kimaiyo alithibitisha.

Mwili wa Bw Ogol baadaye ulipelekwa hospitali ya kaunti ndogo ya Bondo kwa uchunguzi wa maiti huku polisi wakianza uchunguzi kubaini kilichosababisha kifo chake.