"Mtoto anafaa kufaidika!" Sonko amtetea vikali mwanadada anayedai kuwa na mtoto wa Kiptum

Alibainisha kuwa mtoto wa Edna pia anafaa kufaidika na usaidizi wa serikali, kama watoto wengine wa mwanariadha huyo.

Muhtasari

•Sonko alifichua kwamba alinuia kuhudhuria mazishi ya Kiptum ili kumtetea Bi Edna Awour lakini ndege yake ilichelewa.

•“Mimi binafsi nitafadhili na kusapoti michakato muhimu ya kisheria ili kuhakikisha kwamba anapata haki ," Sonko alisema.

Edna Awuor Atieno nje ya mahakama kuu ya Eldoret

Aliyekuwa gavana wa kaunti ya Nairobi, Mike Mbuvi Sonko amejitolea kumsaidia mwanadada wa miaka 22 ambaye anadai kuwa na mtoto na marehemu mwanariadha Kelvin Kiptum katika kupigania haki.

Katika taarifa yake ya Ijumaa, mwanasiasa huyo aliyezingirwa na utata mwingi alifichua kwamba alinuia kuhudhuria mazishi ya Kiptum ili kumtetea Bi Edna Awour lakini ndege yake ilichelewa.

Alibainisha kuwa mtoto ambaye Edna anadai kuwa ni wa Kiptum pia anafaa kufaidika na usaidizi wa serikali, kama watoto wengine wa mwanariadha huyo.

“Issue yangu ilikuwa ni kumtetea huyu mtoto wake na Edna apate Justice just the way I fought for Justice of the late Kibra Mp Ken Okoth’s son na akalipwa all the benefits na bunge na insurance.

Edna’s kid should also be a beneficiary kwa pesa na ile nyumba serikali inapeana. Kwa kuzingatia utetezi wangu wa awali kwa mke wa marehemu Mbunge wa Kibra Ken Okoth kufanyiwa kipimo cha DNA na baadaye kutambuliwa na familia pamoja na mtoto wake, ninajitolea vile vile kutetea haki na kutambuliwa kwa mtoto wa mama wa shujaa wetu Kelvin kiptum. ,” Sonko alisema kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Aliongeza, “Mimi binafsi nitafadhili na kusapoti michakato muhimu ya kisheria ili kuhakikisha kwamba anapata haki na kutambuliwa anakostahili kutoka kwa familia ya mwanariadha huyo. Haki na utu wa kila mtu lazima zidumishwe, na nimejitolea kuona kanuni hiyo ikitekelezwa katika kesi hii.”

Gavana huyo wa zamani anadai kwamba alipanga kutetea haki za mtoto wa Bi Edna kwenye mazishi ya Kiptum ikiwa angefaulu kwenye hafla hiyo.

Pamoja na taarifa yake, alichapisha picha zinazoonyesha marehemu Kiptum akiwa na mwanadada huyo na mtoto wake kama kidokezo kwamba ana haki ya kutafuta sapoti.

Mapema wiki hii, mahakama kuu ya Eldoret ilikataa kusimamisha mazishi ya Kelvin Kiptum kufuatia madai ya Bi Edna Awour kuwa ana mtoto na mwanariadha huyo.

Edna alidai kuwa wako na mtoto ambaye ako mwaka mmoja miezi 7  ambaye haki zake zinaweza kukiukwa ikiwa mazishi hayatasimamishwa.