Mutahi Ngunyi agura upinzani na kuhamia upande wa serikali, aeleza sababu zake

CAS Denis Itumbi alimkaribisha Ngunyi kwenye serikali na kupinga kauli yake kuwa alianzisha mradi wa Hustler Nation.

Muhtasari

•Ngunyi ambaye hapo awali alifanya kazi kama mshauri wa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta kuhusu masuala ya kisiasa alisema hapo awali alikuwa amemhukumu Ruto vibaya.

•Katika majibu yake kwa Ngunyi, Itumbi alibainisha kuwa Hustler Nation ni vuguvugu kubwa ambalo linadhibitiwa na watu. 

Mutahi Ngunyi
Image: MAKTABA

Mchanganuzi mashuhuri wa masuala ya kisiasa Mutahi Ngunyi ametangaza kwamba amehamia upande wa serikali na sasa atamuunga mkono Rais William Ruto.

Wakati akitangaza hatua yake mpya siku ya Jumatatu, Ngunyi ambaye hapo awali alifanya kazi kama mshauri wa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta kuhusu masuala ya kisiasa alisema hapo awali alikuwa amemhukumu Ruto vibaya.

"Taarifa kwa umma: Nimehamia kwa William Ruto. Nilimhukumu vibaya kwa kutumia jicho la nasaba. Lakini ukweli ukibadilika, lazima ubadili mawazo yako," Ngunyi alisema kwenye Twitter.

Aliongeza, "Na mpumbavu pekee ndiye habadili mawazo yake. Nilianzisha mradi wa  #HustlerNation. Sasa lazima niukamilishe. Je, kuna swali? #RutosMountainPlan.”

Hapo awali, Ngunyi alikuwa mkosoaji mkali wa utawala wa Ruto ingawa katika siku za hivi majuzi alijishusha chini na kuanza kumwomba 'kukaa ngumu' (aendelee kuwa na msimamo) hata upande wa upinzani ulipozidisha maandamano ya kupinga serikali mitaani.

Saa chache kabla ya kutangaza kugura upinzani, Ngunyi alikuwa amepongeza mtindo wa uongozi wa Ruto ambao alisema ni wa kimahusiano wala si wa shughuli.

"Siasa za Ruto 'chini' katika Mukurweini. Tofauti kati ya mwanaharakati na rais wa nasaba ni ya moja kwa moja, rais wa nasaba ni ya shughuli huku urais wa Ruto ukiwa ni wa kuhusiana," Ngunyi alisema.

Alikuwa akitoa maoni kwenye klipu ambayo Ruto alionekana akishiriki mazungumzo na wakulima kando ya barabara kuhusu jinsi bora ya kuboresha uzalishaji wa maziwa na kupata faida zaidi.

Miongoni mwa watu waliomkaribisha Mutahi Ngunyi kwa upande wa serikali ni CAS Denis Itumbi ambaye wakati huo huo alipinga kauli ya mshauri huyo wa kisiasa kwamba alianzisha mradi wa Hustler Nation. 

Katika majibu yake kwa Ngunyi, Itumbi alibainisha kuwa Hustler Nation ni vuguvugu kubwa ambalo linadhibitiwa na watu.

“Karibu. Usahihishaji wa haraka, #HustlerNation haijawahi kuwa MRADI. Mradi ndio ulikuwa unasukuma ukashindwa. Nilikuambia mara nyingi sana,” Itumbi alimwambia Ngunyi. 

Aliongeza, "Pili, Hustler Nation ni vuguvugu la watu wengi, sio kitu unachokiendesha hadi kukamilika, watu, kwa fomu yao ya pamoja, wanasimamia. Haya ni mambo muhimu sana unapojiunga. #RutosMountainPlan.