Mwanafamilia anayeshukiwa kutoboa macho ya Baby Sagini kuzuiliwa siku tano

Kesi hiyo itatajwa tena tarehe 23 Disemba.

Muhtasari

•Mahakama imeruhusu Alex Ochogo, 26, kuzuiliwa kwa siku tano zaidi katika Polisi wa Rioma huku wapelelezi wakiendelea na uchunguzi zaidi.

•Mshukiwa alionekana mara ya mwisho akiwa na mtoto huyo kabla ya kugunduliwa akiwa ametobolewa macho.

Ochogo alipokuwa akisindikizwa kurejea katika seli ya polisi ya Rioma baada ya kufika mahakamani Jumatatu
Ochogo alipokuwa akisindikizwa kurejea katika seli ya polisi ya Rioma baada ya kufika mahakamani Jumatatu
Image: MAGATI OBEBO

Mshukiwa mmoja amefikishwa mbele ya mahakama kuhusu kisa cha Alhamisi usiku ambapo mtoto wa miaka 3, Junior Sagini kutoka Marani, Kitutu Chache Kaskazini alipatikana akiwa ameng'olewa macho na watu wasiojulikana.

Hata hivyo, mahakama imeruhusu Alex Ochogo, 26, kuzuiliwa kwa siku tano zaidi katika Polisi wa Rioma huku wapelelezi wakiendelea na uchunguzi zaidi.

Washukiwa wengine zaidi, akiwemo mwanamke mmoja, bado wanasemekana kutoweka huku madaktari katika Hospitali ya Macho ya Kisii wakimruhusu Sagini kuenda nyumbani siku ya Jumapili.

Ogogo alichukuliwa mnamo tarehe 14 mwezi huu na kuzuiliwa katika polisi wa Rioma.

Alifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Christine Ongweno kwa madai ya kujaribu kuua.

Mahakamani, upande wa mashtaka ulisema, mshukiwa alionekana mara ya mwisho akiwa na mtoto huyo kabla ya kugunduliwa akiwa ametobolewa macho.

Mwendesha mashtaka Hillary Kaino aliomba muda zaidi wa kufanya uchunguzi zaidi kuhusu shambulio hilo.

Kesi hiyo itatajwa tena tarehe 23 Disemba.