Mwanafunzi wa chuo kikuu ajitoa uhai baada ya kubet na karo ya Sh15000 kisha kupoteza

Marehemu aliacha barua iliyoelekezwa kwa mama yake ikimwambia abaki na nguvu.

Muhtasari

•Mwanafunzi huyo anasemekana kutumia pesa ambazo zilikusudiwa kulipa karo ya shule kuweka kamari akiwa na matumaini ya kuzizidisha.

Image: HISANI

Mwanafunzi mmoja wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki (CUEA) alijitoa uhai siku ya Jumatano, Machi 27 baada ya kupoteza Sh15,000 katika dau.

Mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 22 anasemekana kutumia pesa ambazo zilikusudiwa kulipa karo ya shule kuweka kamari akiwa na matumaini ya kuzizidisha, lakini kwa bahati mbaya hakushinda na ndipo akaamua kujitoa uhai..

Kisa hicho kinaripotiwa kutendeka katika kijiji cha Raila, eneo la Lang’ata, kaunti ya Nairobi.

Ripoti ya polisi inaonyesha kuwa marehemu aliweka dau hilo siku ya Jumanne usiku na kupoteza. Kisha alionekana mwenye wasiwasi siku iliyofuata kabla ya kuripotiwa kujitoa uhai.

"Mwathiriwa alibaki mwenye wasiwasi siku ya Jumatano mchana na baadaye alijifungia ndani ya nyumba yake na akasikika akizungumza na mtu asiyejulikana," polisi walisema.

Majirani waliokuwa na wasiwasi baadaye walienda kwenye nyumba yake ya kukodi ili kujua jinsi alivyokuwa akijiendelea na kushtuka baada ya kupata mwili wake ukining'inia juu ya paa.

Chifu wa eneo la Muguimoini, George Mukuria alisema maafisa wa polisi walifika Jumatano jioni na kutathmini nyumba hiyo kabla ya kuupeleka mwili wa marehemu katika chumba cha kuhifadhia maiti cha City wakisubiri kufanyiwa  kwa uchunguzi wa maiti.

Marehemu aliacha barua iliyoelekezwa kwa mama yake ikimwambia abaki na nguvu.

Bw Mukuria alibainisha kuwa marehemu huenda alikuwa amekumbwa na msongo wa mawazo baada ya kupoteza pesa mara kwa mara kwa kamari.