Mwili uliotolewa baadhi ya sehemu wapatikana umetupwa barabarani Machakos

"Pia, sehemu zake za siri zilikuwa zimekatwa," afisa mmoja alisema

Muhtasari

•Polisi walisema tukio hilo la Jumapili lilikuwa la mauaji lililofanywa kuonekana kama ajali ya barabarani.

•Maafisa wa upelelezi kutoka kaunti ndogo ya Masinga wameanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo.

Mkusanyiko wa watu karibu na eneo ambapo mwili wa mwanamume mmoja ulipatikana umetupwa kando ya barabara kuu ya Nairobi - Garissa eneo la Kanyonyo, Kaunti ya Machakos mnamo Jumapili, Novemba 13, 2022.
Mkusanyiko wa watu karibu na eneo ambapo mwili wa mwanamume mmoja ulipatikana umetupwa kando ya barabara kuu ya Nairobi - Garissa eneo la Kanyonyo, Kaunti ya Machakos mnamo Jumapili, Novemba 13, 2022.
Image: GEORGE OWITI

Polisi wamefutilia mbali uwezekano wa ajali katika kisa cha mwili uliopatikana ukiwa umelala kando ya barabara kuu ya Nairobi - Garissa, katika kaunti ya Machakos.

Polisi walisema tukio hilo la Jumapili lilikuwa la mauaji lililofanywa kuonekana kama ajali ya barabarani.

Tukio hilo liliripotiwa katika kituo cha Polisi cha Kithyoko katika kaunti ndogo ya Masinga, chini ya OB NO: 5/11/2022 kama tukio la mauaji.

“Iliripotiwa na chifu msaidizi wa eneo hilo Bw. Daniel Nzomo Muthoka kwamba kulikuwa na ajali ya mtu kugongwa na dereva kutoweka kwenye barabara ya Matuu – Kithyoko takriban kilomita 10 Kusini Magharibi mwa kituo hicho. Maafisa kutoka kituoni walitembelea eneo la tukio na kupata maiti ya kijana mmoja akiwa amelala chini na kufunikwa na kitambaa,”sehemu ya ripoti ya polisi ilisomeka.

Polisi walisema walipofika, waliwakuta askari wa trafiki wakiwa tayari kwenye eneo la tukio na ikabainika kuwa haikuwa ajali, bali mauaji yaliyodhaniwa kuwa ajali ya barabarani.

Kwa mujibu wa maafisa hao, mwili huo ulikuwa na majeraha makubwa kichwani na tumboni.

"Pia, sehemu zake za siri zilikuwa zimekatwa," afisa mmoja alisema.

Maafisa wakuu wa polisi kutoka kaunti ndogo ya Masinga wakiongozwa na afisa wa Upelelezi wa Jinai katika eneo hilo walitembelea eneo la tukio.

Mwili wa mwanamume aliyetambuliwa kama Joseph Kyalo Nzui, 42, ulipelekwa hadi katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Mbaku ukisubiri uchunguzi wa maiti.

Maafisa wa upelelezi kutoka kaunti ndogo ya Masinga wameanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo.

Hapo awali, afisa mmoja alikuwa alisema ilishukiwa huenda mwanamume huyo aliuawa kwingine na mwili wake kutupwa barabarani.

"Mwili huu unaweza kuwa umetupwa hapa baada ya kuuawa mahali pengine. Hakuna dalili kwamba aliuawa katika ajali ya barabarani."

Afisa mmoja aliema kwamba waliarifiwa kuhusu mwili huo mwendo wa saa kumi na mbili asubuhi siku ya Jumapili.