Ningeuawa kama si GSU walionilinda- Ledama azungumzia tukio la Bomas

Seneta huyo amewashtumu washirika wa Ruto kwa kumshambulia na kutaka kumwangamiza.

Muhtasari

•Ledama sasa amedai kuwa waliomshambulia ni wafuasi wa Ruto ambao wengi wao ni wabunge wa kuchaguliwa.

•Ametoa shukrani za dhati kwa idara ya polisi kwa usaidizi wao na kwa wote waliochukua hatua ya kumjulia hali.

akizungumza na waandishi wa habari nje ya lango la Bomas mnamo Jumatatu, August 15 2022.
Seneta wa Narok Ledama Ole Kina akizungumza na waandishi wa habari nje ya lango la Bomas mnamo Jumatatu, August 15 2022.
Image: HISANI

Seneta wa kaunti ya Narok Ledama Ole Kina amewashtumu washirika wa rais mteule William Ruto kwa kumshambulia.

Jumatatu video iliyoonyesha mwanasiasa huyo akijaribu kutoroka ukumbi wa Bomas huku umati wa watu ukionekana kumshambulia  kwa ngumi na mateke ilisambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

Ledama sasa amedai kuwa waliomshambulia ni wafuasi wa Ruto ambao wengi wao ni wabunge wa kuchaguliwa.

"Nilishambuliwa kikatili na wafuasi wa  William Ruto wengi wao waliochaguliwa kuwa wabunge katika Bomas of Kenya wakipiga kelele muueni! muueni!. GSU walinilinda la sivyo ningeuawa," Ledama alisema kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Seneta huyo aliyechaguliwa kwa muhula wa pili hata hivyo hakutoa maelezo zaidi wala kuficha mtu yeyote aliyehusika.

Ametoa shukrani za dhati kwa idara ya polisi kwa usaidizi wao na kwa wote waliochukua hatua ya kumjulia hali.

"Asante @NPSOfficial_KE Ninashukuru kwa kila mtu ambaye amepiga simu kuniangalia!" Alisema.

Katika video iliyosambazwa mapema wiki hii, Ledama ambaye ni miongoni mwa wanasiasa waliokuwa wamejumuika Bomas kufuatilia matokeo ya urais alionekana akiwa akishambuliwa na wasiojulikana.

Akizungumza na wanahabari baada ya mashambulizi hayo, Ledama alidai kuwa mwili wake mkubwa ndio ulimsaidia kugura eneo la hatari. 

"Alituma wahuni na GSU kuja kutushambulia. Niko na bahati kwa kuwa mimi ni mkubwa, la sivyo wangeniangamiza. Hii nchi ni kubwa kuliko pesa. Hatutaruhusu yoyote mabaya kufanyika huku," Alisema.

Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alisema makamishna wawili wa tume walijeruhiwa katika vurugu hivyo.

Jumatano, Chebukati alisema kisa hicho kimeathiri makamishna na kupelekea kuahirishwa kwa uchaguzi katika maeneo ambayo upigaji kura haukufanyika.

"Hii imezua hofu kwa wafanyikazi ambao sasa hawawezi kuripoti afisi kazini," Chebukati alisema.

“Tunatoa wito wa kukamatwa na kufunguliwa mashtaka dhidi ya wavamizi hawa bila kujali itikadi zao za kisiasa,” aliongeza.