Polisi wapata mizoga ya punda iliyokusudiwa kuuzwa Nairobi, washukiwa 3 watoroka

Baada ya kufika eneo la uhalifu, polisi walikuta mizoga zaidi ya saba ikiwa imetapakaa chini.

Muhtasari

•Mizoga  ya punda waliochinjwa iliyokuwa ikitayarishwa kwa matumizi ilipatikana usiku wa kuamkia siku ya Jumanne.

•DCI walidai kuwa nyama ya wanyama wanaochinjwa katika eneo la uhalifu kawaida huuzwa kwa wakaazi wa jiji la Nairobi ambao huwa wanaifurahia sana.

Image: TWITTER// DCI

Polisi katika kaunti ya Kiambu wanawasaka washukiwa watatu waliotoroka baada ya mizoga ya punda kupatikana kwenye kichaka.

Kurugenzi ya Uchunguzi wa Jinai imeripoti kuwa mizoga  ya punda waliochinjwa iliyokuwa ikitayarishwa kwa matumizi ya eneo hilo ilipatikana usiku wa kuamkia siku ya Jumanne kufuatia operesheni ambayo ilifanyika katika kichinjio kilicho katika Kijiji cha Kiahiti, kitongoji cha Gatune, Kaunti ya Kiambu.

Baada ya kufika eneo hilo kufuatia taarifa za kijasusi za uhalifu huo, polisi walikuta mizoga zaidi ya saba ikiwa imetapakaa chini.

“Hapo awali polisi wa kituo cha Nachu walikuwa wamekusanya taarifa za kipelelezi juu ya  kuchinja huko  kulikotarajiwa na wakafika eneo la tukio kwa wakati huku wauzaji hao wa nyama wabaya wakiwachinja wanyama hao ambao nyama zao huingia kwenye mabucha ya nyama jijini ikidaiwa kuwa  nyama ya ng'ombe.

Wakaazi wa eneo la Kiahiti walikuwa wamelalamikia usingizi wao kutatizwa na milio ya punda wakihangaika; ho, hii, hoo hiiii, hooo hiiiii, brrrrrr!!!! walipokuwa wakiongozwa hadi eneo la tukio kukabiliana na shoka,” taarifa ya DCI ilisema.

Maafisa walioendesha operesheni hiyo pia waligundua kuwa baada ya kuwachinja punda hao, wafanyabiashara hao huchukua nyama isiyo na mfupa kutoka kwa mizoga  ambayo baadaye huuzwa jijini ikidaiwa kuwa minofu ya ng’ombe na nyama ya ngomb’e zisizo na mfupa.

"Hakuna nyama inayoachwa ipotee kwani wafanyibiashara pia hufunga matumbo ya punda, figo na viungo vingine vya ndani ambavyo huuzwa kwenye maduka yanayouza vyakula vya kitamu, mutura, supu na matumbo," ilisema taarifa hiyo.

DCI walidai kuwa nyama ya wanyama wanaochinjwa katika eneo la uhalifu kawaida huuzwa kwa wakaazi wa jiji la Nairobi ambao huwa wanaifurahia sana.

Msako wa kuwatafuta washukiwa waliotoroka eneo la tukio unaendelea, DCI iliripoti.