Seneta Ledama Olekina hatimaye amjibu Mercy Tarus baada ya kukataa ofa yake ya kazi

Ledama alibainisha kuwa hakumpa mwanadada huyo kazi badala yake alisema tu kwamba angependa amfanyie kazi.

Muhtasari

•Ledama alisema kuwa anaheshimu uamuzi wa mhitimu huyo wa Chuo Kikuu cha Kabarak kwani ana haki ya kujibu vile.

•Mercy aliataa kazi hiyo na kutoa masharti ya kutimizwa kabla ya kukubali kufanya mazungumzo na mwanasiasa huyo.

LEDAMA 2
LEDAMA 2

Seneta wa Narok Ledama Olekina hatimaye amejibu baada ya mwanadada Mercy Tarus kukataa ofa yake ya kazi siku chache zilizopita.

Katika taarifa yake ya Jumamosi, mwanasiasa huyo ambaye alifurahishwa sana na ujasiri wa Mercy aliposimama kuwazomea vikali viongozi wa Uasin Gishu mapema wiki hii kuhusu mpango uliofeli wa elimu ya ng'ambo alisema kwamba anaheshimu uamuzi wa mhitimu huyo wa Chuo Kikuu cha Kabarak kwani ana haki ya kujibu vile.

Wakati huohuo, Ledama alibainisha kuwa hakumpa mwanadada huyo kazi badala yake alisema tu kwamba angependa amfanyie kazi.

"Ikiwa kweli jibu lilitoka kwa Mercy Tarus, ana haki ya kujibu hivyo na ninaheshimu hisia zake. Msimamo wangu ulikuwa wazi, nilisema ningependa anifanyie kazi! Kupenda na kutoa kuna maana mbili tofauti,” Ledama alisema.

Seneta huyo wa ODM aliongeza, “Ninapenda ujasiri wake na tabia yake ya uwazi na ambayo inaweza kuwavutia wafanyikazi wengine. Sasa linapokuja suala la kutoa kazi, hiyo inaweza kuwa ya pili kwa masharti maalum au mwaliko wa kufanya kazi kwa jukumu maalum la kulipwa.”

Siku ya Alhamisi, Ledama alimsifu mhitimu huyo wa Chuo Kikuu cha Kabarak kwa ujasiri wake na kumpa nafasi ya kumfanyia kazi.

“Mercy Tarus ningependa unifanyie kazi, speka moyo wako. Wakati ujao ni wa vijana waaminifu! Wacha tuzungumze,” Ledama aliambia mwanadada huyo kupitia mtandao wa Twitter.

Huku akimjibu seneta huyo, Mercy hata hivyo alionekana kukataa kazi hiyo na kutoa masharti ya kutimizwa kabla ya kukubali kufanya mazungumzo na mwanasiasa huyo.

Mhitimu huyo wa chuo kikuu alimtaka seneta Ledama kwanza kuwaomba maseneta wenzake kuishinikiza serikali ya Uasin Gishu kurejesha pesa ambazo walikuwa wamepokea kutoka kwa wazazi kwa ajili ya mpango wa masomo wa ng’ambo uliofeli.

"Bwana. Ledama, kabla hatujaendeleza mazungumzo haya, zungumza na maseneta wenzako ili kuwajibisha Serikali ya Kaunti ya Uasin Gishu na kuwalazimisha KUREJESHA pesa zilizopatikana kwa bidii kwa Raia wa Kenya. Labda baadaye, tunaweza kuzungumza. Vinginevyo, sina la kusema zaidi,” Mercy alijibu siku ya Alhamisi.

Mercy alidokeza kuwa hayuko tayari kufanya kazi na seneta huyo wa ODM kwa sasa lakini akadokeza kuwa katika siku zijazo huenda akakubali ofa ya kazi kutoka kwake.

"Labda basi, tunaweza kufanya kazi kwenye mradi unaofuata kwa sababu kazi yangu itafanyika hapa. Vinginevyo, siwezi kujitolea kwa majukumu mengine," alisema.