•Alionekana mwenye wasiwasi mwingi na mwenye haraka wakati akiingia dukani na kumpa muhudumu wa duka hilo simu yake.
•Maafisa wa upelelezi wamechukua picha hizo za CCTV kwa uchunguzi zaidi na wanazitumia kumtambua mshukiwa.
Huku uchunguzi kuhusu mauaji ya kikatili ya mwanamke mwenye umri wa miaka 24 katika eneo la TRM Drive, mtaa wa Kasarani ukiendelea, wapelelezi wanaoshughulikia kesi hiyo wamefanikiwa kupata video za CCTV zinazoonyesha picha za mshukiwa wa unyama huo.
Katika picha za CCTV zilizofikia Radio Jambo, mshukiwa alionekana akifika kwenye duka moja la eneo hilo ambapo inasemekana alikuwa ameambiwa achukue funguo za chumba cha Airbnb ambacho alikuwa amelipia. Alionekana mwenye wasiwasi mwingi na mwenye haraka wakati akiingia dukani na kumpa muhudumu wa duka hilo simu yake ili aongee na mwenye chumba cha AirBnB alichokuwa amepanga na apatiwe idhini ya kumpa funguo.
Mshukiwa ambaye alikuwa amevalia kofia nyeupe na kushikilia begi mikononi mwake wakati wote huo bado alionekana kuwa na wasiwasi wakati mhudumu wa duka alikuwa akizungumza na mmiliki wa AirBnB kwenye simu.
Punde baada ya kukabidhiwa simu yake na funguo, mtuhumiwa alionekana akitoka nje ya duka hilo kwa haraka kisha kutoweka. Inaripotiwa kuwa hakuwahi kurudisha funguo alizochukua.
Maafisa wa upelelezi wamechukua picha hizo za CCTV kwa uchunguzi zaidi na wanazitumia kumtambua mshukiwa ili waweze kumtia mbaroni.
Uchunguzi zaidi umebaini kuwa mshukiwa wa mauaji hayo ya kikatili alitumia laini ya Airtel kuwasiliana na mmiliki wa AirBnB kabla ya kuelekea chumbani ambako alimfanyia kitendo hicho cha kinyama mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 24.
Familia ya marehemu ilifika katika chumba cha kuhifadhi maiti cha City jijini Nairobi siku ya Jumatatu ambapo walitambua mwili wa jamaa wao. Hata hivyo walikwepa kuzungumza na vyombo vya habari wakisema wanasubiri polisi kukamilisha uchunguzi wao kabla ya kutoa taarifa yoyote.