Tanzia! Bingwa wa marathon, Kelvin Kiptum afariki katika ajali ya barabarani

Alifariki pamoja na kocha wake, Gervais Hakizimana wa Rwanda, katika ajali iliyotokea kwenye barabara magharibi mwa Kenya.

Muhtasari

•Ajali hiyo ya barabarani ilitokea mwendo wa saa  tano usiku, kwa saa za Kenya  (20:00 GMT) siku ya Jumapili.

•Kiptum aliandikisha mafanikio mnamo 2023 kama mpinzani wa mwenzake Eliud Kipchoge - mmoja wa wanariadha wakuu wa marathon.

Kelvin Kiptum amefariki
Mwanariadha Kelvin Kiptum amefariki
Image: BBC

Mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mbio za marathon za wanaume, Mkenya Kelvin Kiptum, 24, amefariki dunia katika ajali ya barabarani.

Alifariki pamoja na kocha wake, Gervais Hakizimana wa Rwanda, ndani ya gari kwenye barabara magharibi mwa Kenya siku ya Jumapili.

Kiptum aliandikisha mafanikio mnamo 2023 kama mpinzani wa mwenzake Eliud Kipchoge - mmoja wa wanariadha wakuu wa marathon.

Na ilikuwa Chicago Oktoba mwaka jana ambapo Kiptum aliboresha mafanikio ya Kipchoge,akimaliza umbali wa maili 26.1 (42km) kwa saa mbili na sekunde 35.

Wanariadha hao wawili walikuwa wametajwa katika timu ya Kenya ya marathon kwa ajili ya Michezo ya Olimpiki ya Paris baadaye mwaka huu.

Akitoa risala zake kwa Kiptum, Waziri wa Michezo wa Kenya Ababu Namwamba aliandika kwenye X: "Inasikitisha sana!! Kenya imepoteza vito maalum. Sina la kusema."

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya na waziri mkuu wa zamani, Raila Odinga, alisema nchi hiyo imepoteza "shujaa wa kweli" na inaomboleza "mtu wa ajabu... na kinara wa riadha wa Kenya".

Sebastian Coe, rais wa Riadha Duniani, alisema Kiptum "ni mwanariadha wa ajabu aliyeacha historia ya ajabu, tutamkosa sana".

Ajali hiyo ya barabarani ilitokea mwendo wa saa 23:00 kwa saa za Kenya  (20:00 GMT) siku ya Jumapili, polisi walinukuliwa wakisema na shirika la habari la AFP.

Wakitoa maelezo zaidi kuhusu ajali hiyo, polisi walisema Kiptum ndiye aliyekuwa dereva, na gari "lilipoteza mwelekeo na kubingiria na kuwaua wawili hao papo hapo".

Msemaji aliyenukuliwa na AFP aliongeza kuwa abiria wa tatu - ambaye alikuwa mwanamke - amejeruhiwa na "kukimbizwa hospitali".

Wiki iliyopita tu, timu yake ilitangaza kwamba angejaribu kukimbia umbali wa chini ya saa mbili katika mbio za marathon za Rotterdam - hatua ambayo haijawahi kuafikiwa katika mashindano ya wazi.

Ukuaji wa umaarufu wa baba huyo wa watoto wawili ulikuwa wa haraka - alikimbia marathon yake ya kwanza kamili mnamo 2022.

Alishiriki katika shindano lake kuu la kwanza miaka minne iliyopita akikimbia kwa viatu vya kuazima kwani hakuweza kumudu jozi yake mwenyewe.

Alikuwa miongoni mwa wanariadha wapya wa Kenya ambao walianza uchezaji wao ugenini, wakiachana na tamaduni ya zamani ya wanariadha kuanza kwenye mbio kabla ya kuhamia masafa marefu.

Kiptum aliiambia BBC mwaka jana kwamba chaguo lake lisilo la kawaida liliamuliwa tu na ukosefu wa rasilimali.

“Sikuwa na pesa za kusafiri kufuatilia vikao,” alieleza.

Kocha wake, Hakizimana, 36, alikuwa mwanariadha mstaafu wa Rwanda. Mwaka jana, alitumia miezi kadhaa kumsaidia Kiptum kulenga rekodi ya dunia.

Uhusiano wao kama kocha na mwanariadha ulianza mnamo 2018, lakini wawili hao walikutana kwa mara ya kwanza wakati mshikilizi huyo wa rekodi ya ulimwengu alipokuwa mchanga zaidi.

"Nilimfahamu alipokuwa mvulana mdogo, akichunga mifugo bila viatu," Hakizimana alikumbuka mwaka jana. "Ilikuwa mwaka wa 2009, nilikuwa nikifanya mazoezi karibu na shamba la baba yake, alikuja kunipiga teke na nikamfukuza.

"Sasa, ninamshukuru kwa mafanikio yake."