"Tunatangaza njaa!" Mwandamanaji afichua sababu ya kuvaa taulo, kuandamana na mwanawe

"Hatuna mawe, hatuna silaha yoyote, sisi tunatangaza njaa tu,” Erick alisema.

Muhtasari

•Victor Erick alisindikizwa na mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka mitatu ambaye pia alijifunga taulo.

•Erick alisema haogopi kubeba mwanawe kwenye maandamano kwa sababu ni ya amani na kubainisha hawakuwa wamebeba silaha.

wakati wa maandamano ya Azimio mjini Kisumu mnamo Machi 27, 2023.
Victor Erick na mwanawe wa miaka mitatu wakati wa maandamano ya Azimio mjini Kisumu mnamo Machi 27, 2023.
Image: DANIEL OGENDO

Mfuasi mmoja wa muungano wa Azimio La Umoja-One Kenya aliandamana barabarani kulamikia gharama ya juu ya maisha nchini.

Huku akiwa amejifunga taulo kiunoni na mswaki mdomoni, mwanaume huyo aliyetambulika kwa jina Victor Erick alisindikizwa na mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka mitatu ambaye pia alijifunga taulo.

Erick alionekana akitembea katika barabara za jiji la Kisumu na pamoja mwanawe, huku akiwa ameshikilia bango.

Bango hilo lilikuwa limeandikwa, "Azimio inasema hapana kwa gharama ya juu ya maisha."

Erick alisema haogopi kubeba mtoto wake katika maandamano kwa sababu ni ya amani na kubainisha hawakuwa wamebeba silaha.

“Mimi huwa nafunga taulo hivi, hata siku ya kupiga kura nilifunga hivi, hivi ndivyo mimi najivaa,” alisema.

Erick alipoulizwa kwa nini aliamua kumbeba mtoto huyo wake wa kwanza kwenye maandamano na ikiwa alikuwa na wasiwasi wowote kuhusu usalama wake alisema, “Hatuna wasiwasi kwa sababu sio eti maandamano ina mawe, umeona tumebeba mawe hapa? Hatuna mawe, hatuna silaha yoyote, sisi tunatangaza njaa tu.”

Siku ya Jumapili, Inspekta Jenerali Japhet Koome alitoa onyo kali dhidi ya mikusanyiko yoyote ya watu wengi ama maandamano huku akibainisha kuwa ni kinyume cha sheria.

Koome alitishia kuwakamata viongozi wakuu, ikiwa ni pamoja na kiongozi wa upinzani Raila Odinga ikiwa watajaribu kufanya maandamano siku ya Jumatatu na Alhamisi. Aliweka wazi kuwa makamanda wake hawatajali hadhi ya mtu yeyote katika jamii wanapokabiliana na waandamanaji.

"Hata iwe ni nani, nitakushughulikia," Koome alisema.

Huku akimjibu Koome, kiongozi wa Azimio Raila Odinga alitangaza kwamba hatarudi nyuma kamwe kuhusu maandamano ya Jumatatu na kumthubutu bosi huyo wa polisi kupiga hatua ya kumkamata yeye mwenyewe.

"Bwana Koome, koma kabisa hapo kesho. Umesema utanishika mimi. Niko tayari kukamatwa. Usitume askari, njoo wewe mwenyewe unikamate. Nitakuwa mstari wa mbele tuonane ana kwa ana,” Alisema.