"Usitume askari, njoo mwenyewe unikamate!" Raila amwambia Inspekta Jenerali Koome

Raila alibainisha kwamba maandamano ya Jumatatu yataendelea kama yalivyoratibiwa.

Muhtasari

•Siku ya Jumapili, Koome alionya dhidi ya mikusanyiko yoyote ya watu wengi ama maandamano wakisema kuwa ni kinyume cha sheria.

•Waziri mkuu huyo wa zamani aliweka wazi kwamba yuko tayari kutiwa mbaroni na kumtaka Koome amtie pingu mwenyewe.

baada ya kuhudhuria ibada ya Jumapili katika JTM mnamo Machi 26, 2023.
Kiongozi wa Azimio Raila Odinga baada ya kuhudhuria ibada ya Jumapili katika JTM mnamo Machi 26, 2023.
Image: TWITTER//RAILA ODINGA

Kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga amemjibu Inspekta Jenerali Japheth Koome baada ya kutishia kuwakamata viongozi wakuu wa Azimio ikiwa watajaribu kufanya maandamano siku ya Jumatatu na Alhamisi.

Siku ya Jumapili, Koome alionya dhidi ya mikusanyiko yoyote ya watu wengi ama maandamano wakisema kuwa ni kinyume cha sheria.

Alisema kwamba polisi watawatendea watu kwa usawa wakati wa kuwakamata waandamanaji mitaani huku akiweka wazi kuwa hata makamanda wake hawatajali hadhi ya mtu yeyote katika jamii wanapokabiliana na waandamanaji.

"Hata iwe ni nani, nitakushughulikia," Koome alisema.

Katika jibu lake kwa bosi huyo wa polisi, Raila alibainisha kwamba maandamano ya Jumatatu yataendelea kama yalivyoratibiwa.

Waziri mkuu huyo wa zamani aliweka wazi kwamba yuko tayari kutiwa mbaroni na kumtaka Koome amtie pingu mwenyewe.

"Bwana Koome, koma kabisa hapo kesho. Umesema utanishika mimi. Niko tayari kukamatwa. Usitume askari, njoo wewe mwenyewe unikamate. Nitakuwa mstari wa mbele tuonane ana kwa ana,” Alisema.

Kiongozi huyo wa Upinzani alizungumza wakati wa ibada ya kanisa la JTM, katika mtaa wa Embakasi, Nairobi.

Aliwashtumu maafisa wa polisi wa Kenya kwa kukosa utu kufuatia jinsi wanavyowashughulikia waandamanaji.

"Polisi wa Kenya wanafanya kama polisi wa kikoloni. Masomo yao bado yako katika mazingira ya ukoloni. Hawana utu sana," alisema.

IG Koome alisema kuwa hakutakuwa na utaratibu maalum kwa mtu yeyote wakati wa kuwakamata waandamanaji ikiwa ni pamoja na wale ambao watakuwa wamebebwa kwenye magari makubwa kama Prado.

"Hata uwe kiwango gani katika jamii, uwe katika hadhi gani. Nina land cruiser za kutosha kukuweka upande wa nyuma. Kesho siweki mtu kwenye Prado. Nitakayemkamata kesho nitakuweka kwenye Landcruiser, utakwenda jela na kukaa huko milele," alisema.

Alisema yeyote atakayekutwa na silaha za kushambulia na kusababisha fujo atachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria.

Koome alisema silaha za mashambulizi ni pamoja na mawe, rungu, panga pamoja na zana zingine.

"Ikiwa una nia ya kusababisha fujo, na umejihami kwa kile tunachoita silaha za kudhuru, mawe, rungu na mapanga utakabiliwa nawe," Koome alisema.