Brazil yaibandua Argentina kwenye michuano ya Copa america

Brazil ilicharaza Argentina magoli mawili bila jibu uwanjani Estadio Mineirao jana usiku. Mshambulizi wa Manchester City, Gabriel Jesus alifungua ukurasa mnamo dakika ya kumi na tisa baada ya kupokea pasi murua kutoka kwake Firmino.

Hata hivyo, Argentina ilitawala mchezo mzima huku ikishuhudia mashuti yake mawili yakigonga mwamba. Sergio Aguero aligonga mwamba mnamo dakika ya 26 huku Lionel Messi akifanya vivo hivyo mnamo dakika ya 65.

Roberto Firmino aliwaamsha tena mashabiki wa nyumbani kunako dakika ya 71 alipotia msumari wa mwisho kwenye jeneza la Argentina kwa kuliweka goli la pili upande wa Brazil. Firmino akiwa ndiye mchezaji bora kwenye mechi hio alipata goli lake la pili kwenye michuano hio.

Brazil imejikatia tiketi ya kucheza fainali za Copa America kwa mara ya kwanza tangu mwaka wa 2007.

Bingwa mtetezi Chile akiongozwa na winga wa Manchester United, Alexis Sanchez, itakua dimbani hii leo kukipiga dhidi ya Peru kwenye nusu fainali ya pili uwanjani Arena Do Gremio.

Brazil inangoja mshindi baina ya Chile na Peru kwenye fainali huku Argentina ikingoja atakayepoteza ili kuiwania nafasi ya tatu.

Fainali za Copa America zitachezwa tarehe saba mwezi huu.

Kwingineko, Mexico ilifika kwenye fainali ya CONCACAF gold baada ya kuinyuka Haiti goli moja bila jibu. Mshambulizi wa Wolves ya Uingereza, Raul Jimenez, alitia kimiani goli la kipekee kunako dakika ya 93 kupitia njia ya penalti.

Hii leo, U.S.A itamkaribisha Jamaica kwenye nusu fainali ya pili.