Wageni waheshimiwa wahudhuria misa ya wafu ya Joe Kadenge

Magwiji wa kadanda nchini, wanasiasa, familia na marafiki wa mwenda zake Joe Kadenge ni miongoni mwa mamia ya waliohudhuria misa yake ya wafu katika kanisa la Friends Church, Ngong road.

Gwiji huyo wa kadanda nchini, aliaga dunia yapata wiki mbili zilizopita akiwa na umri wa miaka 84, na alisifiwa na wengi kama mwanasoka ambaye aliiletea Kenya hadhi kuu katika nyanja ya soka.

Miongoni mwa waliohudhuria misa hiyo ni rafiki wake wa karibu, mtangazaji Jacob 'Ghost' Mulee, kinara wa ODM, Raila Odinga, mwenzake wa Ford Kenya, Musalia Mudavadi na mwakilishi wa kina mama kaunti ya Nairobi, Esther Passaris.

Joe Kadenge alikuwa mwanasoka mahiri sana siku zake na aliichezea timu ya taifa Harambee stars kwa miaka 14 baada ya kuanza kusakata boli  miaka ya sitini.

Baada ya kustaafu kutoka soka, Joe alijitosa katika usimamizi wa kandanda ambapo pia alipaa na kuwa kocha wa timu ya Harambee Stars mwaka wa 2002.

Mwenyezi mungu na aijalie nafsi yake na kuipa ujasiri familia na rafiki zake.