Beki wa Liverpool Van Dijk ndiye mchezaji bora bara ulaya

Beki wa Liverpool na Uholanzi Virgil van Dijk amewabwaga magwiji Cristiano Ronaldo na Lionel Messi ma kushinda tuzo la mchezaji bora wa bara Ulaya mwaka 2018/19.

Van Dijk ni mchezaji wa pili kuwapiku nyota hao ambao wametamba kwa zaidi ya muongo mmoja uliopita, baada ya Luka Modric kufanikiwa kuwabandua mwaka uliopita. Van Dijk aliiongoza safu ya ulinzi ya Liverpool kutwaa taji la ligi ya mabingwa msimu uliopita.

Kiungo wa Manchester United Alexis Sanchez amejiunga na Inter Milan kwa mkopo. Raia huyo wa Chile atasalia na kikosi cha Antonio Conte hadi Juni mwaka wa 2020.

Sanchez atakutana na mchezaji mwenzake wa zamani wa United Romelu Lukaku, ambaye alijiunga na Inter mwezi uliopita. Sanchez ndie mchezaji anayelipwa kitita kikubwa cha fedha Old Trafford, na inaaminika kwamba United wanalipa sehemu ya mshahara wake takriban pauni elfu 400 kwa wiki ili kuruhusu uhamisho huo.

Kiungo wa kati wa Manchester United na timu ya taifa ya Ufaransa Paul Pogba, mwenye umri wa miaka 26, hatoongeza mkataba wake hivi sasa na anataka kujiunga na Real Madrid haraka iwezekanavyo. Kwingineko, Paris St-Germain inamtaka kiungo wa kati wa Tottenham Christian Eriksen mwenye umri wa miaka 27, kama mchezaji atakayeichukua nafasi ya mchezaji wa timu ya taifa ya Brazil Neymar, anayekaribia kurudi Barcelona.

Tottenham wanaripotiwa kukubaliana mkataba wa kumuuzaVictor Wanyama kwa klabu ya Ubelgiji Brugge kwa kitita cha pauni milioni 12.

Kiungo huyo wa kati wa umri wa miaka 28 hajachezea Spurs mechi hata moja msimu huu na sasa ameamua kuhamia Uropa ambapo dirisha la uhamisho liko wazi hadi mwanzo wa mwezi Septemba.

Wanyama alijiunga na Spurs kutoka Southampton mwaka 2016 na amewachezea mechi 93.