Wanawake 4 kuweka historia ya kusimamia Mechi ya Afcon leo

Muhtasari
  • Wanawake 4 kuweka historia ya kusimamia Mechi ya Afcon leo
Image: Afcon Twitter

Mwamuzi mzaliwa wa Rwanda, Salima Rhadia Mukansanga ataweka historia saa chache zijazo atakapokuwa mwanamke wa kwanza kuwa muamuzi katika mechi ya timu za wanaume kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika.

Mukansanga, 35, atasimamia mechi ya hatua ya makundi kati ya Zimbabwe na Guinea Jumanne,itakayopigwa leo kwenye Uwanja wa Ahmadou Ahidjo mjini Yaounde.

Yeye ni sehemu ya timu ya marefa wa kike iliyochaguliwa kama maafisa wa mechi kwenye mechi hiyo - na hivyo kuwa mara ya kwanza kabisa kwa timu ya wanawake wote kusimamia mechi katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika tangu mashindano hayo kuanzishwa. wasaidizi wake watakuwa ,Carine Atemzabong (Cameroon) na Fatiha Jermoumi (Morocco) pamoja na mwamuzi wa VAR Bouchra Karboubi (Morocco).

Tarehe 10 Januari 2022, Mukansanga aliweka historia kwa kuwa mwanamke wa kwanza kusimamia mechi katika Kombe la Mataifa ya Afrika –nchini Cameroon alipoteuliwa kuwa afisa wa nne katika mchezo kati ya Guinea na Malawi mjini Bafoussam.

Mkuu wa Waamuzi wa CAF, Eddy Maillet alisema kwa vyombo vya habari kuwa wakati huu wa kihistoria ni matokeo ya dhamira ya wazi ya CAF na uwekezaji wa kuboresha na kuendeleza kiwango cha waamuzi barani Afrika.

Hii ikiwa ni sehemu ya mpango unaofahamika kama ‘Star Programme’ iliyoanzishwa na FIFA na CAF kuendeleza waamuzi. Maillet alisema: “Tunajivunia sana Salima kwa sababu amelazimika kufanya kazi kwa bidii ili kuwa hapa alipo leo.

Tunajua kwa mwanamke amelazimika kushinda vikwazo vizito kufikia kiwango hiki na anastahili pongezi nyingi. Wakati huu si kwa Salima pekee bali ni kwa kila msichana mdogo barani Afrika mwenye mapenzi ya soka na anayejiona kuwa mwamuzi siku za usoni.