Mwanariadha Mkenya Pamela Jelimo apokea medali ya Olimpiki miaka 10 baadaye

Pamela Jelimo alisema kusubiri miaka mingi ilikuwa chungu

Muhtasari

•Jelimo alipewa nishani hiyo kufuatia IOC kumuondoa Mariya Savinova wa Urusi kwenye mashindano hayo kutokana na ukiukaji wa matumizi ya dawa za kusisimua misuli.

Pamela Jelimo alisema kusubiri miaka mingi ilikuwa chungu
Pamela Jelimo alisema kusubiri miaka mingi ilikuwa chungu
Image: BBC

Miaka kadhaa baada ya kumaliza wa nne katika fainali ya mita 800 kwenye Michezo ya Olimpiki ya 2012 jijini London, Mkenya Pamela Jelimo amepokea medali ya shaba.

Jelimo, almaarufu Eldoret Express, alipewa nishani hiyo kufuatia Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) kumuondoa Mariya Savinova wa Urusi kwenye mashindano hayo kutokana na ukiukaji wa matumizi ya dawa za kusisimua misuli mwaka wa 2015.

Savinova alishinda medali ya dhahabu ya mita 800 mwaka wa 2012. Akizungumza na BBC, Jelimo alilaani matumizi ya dawa za kusisimua misuli katika michezo, akisema ni "tishio kwa mwanariadha kuendeleza ujuzi wake kitaaluma", "Hii ni kama ndoto. Hapo awali sikuamini niliposikia habari hizi njema. Hakika ni ndoto ya kila mwanariadha kushinda medali katika Olimpiki na nina furaha kuwa na wazazi wangu kunisindikiza na kushiriki furaha hii.”

Sherehe ya aina hii inajiri wakati ambapo Kenya imeangaziwa kutokana na visa vingi vya utumiaji dawa za kusisimua misuli na hivi majuzi nusra ikumbane na marufuku ya kimataifa.