Kipchoge avunja kimya baada ya kumaliza wa sita katika mbio za Boston Marathon

Kipchoge amekubali kwamba jana, Aprili 17, haikuwa siku nzuri kwake katika mbio za Boston Marathon.

Muhtasari

•Kipchoge alimaliza wa sita katika shindano hilo ambalo lilitwaliwa na mwanariadha mwingine wa Kenya, Evans Chebet.

•Kipchoge aliwapongeza washindani wake wote katika mbio hizo na kutoa shukrani za dhati kwa wote waliompa sapoti.

alimaliza wa sita katika Boston Marathon.
Kipchoge alimaliza wa sita katika Boston Marathon.
Image: TWITTER// ELIUD KIPCHOGE

Bingwa wa mbio za masafa marefu Eliud Kipchoge amekubali kwamba jana, Aprili 17, haikuwa siku nzuri kwake katika mbio za Boston Marathon.

Kipchoge alimaliza wa sita katika shindano hilo ambalo lilitwaliwa na mwanariadha mwingine wa Kenya, Evans Chebet aliyekamilisha mbio hizo kwa saa 2:05:54. Mwanariadha Gabriel Gaey kutoka nchi jirani ya Tanzania alimaliza katika nafasi ya pili huku Benson Kipruto akiipatia Kenya nishani ya shaba.

Bingwa huyo wa mbio hizo mara kadhaa aliweka wazi kwamba aliyapa mashindano ya Boston  ubora wake wote lakini kwa bahati mbaya juhudi zake hazikuzalisha matokeo yaliyotarajiwa na wengi.

"Ninaishi kwa wakati ambapo ninatoachangamoto kwa mipaka. Haijahakikishiwa kamwe, sio rahisi kamwe. Leo ilikuwa siku ngumu kwangu. Nilijikaza kadri niwezavyo lakini wakati mwingine, lazima tukubali kwamba leo haikuwa siku ya kusukuma kizuizi kwa urefu zaidi," alisema baada ya mbio hizo.

Kipchoge aliwapongeza washindani wake wote katika mbio hizo na kutoa shukrani za dhati kwa wote waliompa sapoti.

"Katika michezo unashinda na unashindwa na daima kuna kesho kuweka changamoto mpya. Nafurahi kwa kile kilicho mbele," alisema.

Mamia ya mashabiki wake kote ulimwenguni walikusanyika ili kumfariji na kumtia moyo katika safari iliyoko mbele yake.

Siku ya Jumatatu jioni, Kipchoge alistahimili hali ya mvua na upepo katika jiji la Boston na kushika nafasi ya sita kwa kutumia saa 2:09:23.

Huku Kipchoge akihangaika, Evans Chebet alitetea taji lake kwa kutimua mbio katika kilomita ya mwisho na kumaliza kwa saa 2:05:04.

Mtanzania Gabriel Gray alionyesha ubora wake na kumaliza wa pili kwa saa 2:06:04 huku Benson Kipruto akimaliza nafasi za tatu kwa saa 2:06:06.

Albert Korir aliibuka wa nne kwa saa 2:08:01 huku Talbi Zouhair wa Morocco akimaliza wa tano kwa saa 2:08:35.

Chebet alifurahishwa na ushindi huo ambao alipata licha ya hali ya mvua ya vipindi na hali ngumu.

“Nina furaha leo. Ikiwa imesalia kilomita moja, nilijiamini kwenda njia yote na kushinda," Chebet alisema.

Kwa Kipchoge, zilikuwa mbio zake za tatu mbaya zaidi tangu ajiunge na mbio za marathon mwaka wa 2013.

Alimaliza wa nane kwenye mbio za London Marathon za 2020 ambapo alitumia saa 2:06:49. Katika mbio za Berlin Marathon za 2013, aliibuka wa pili kwa saa 2:04:05, nyuma ya Wilson Kipsang katika rekodi ya dunia ya wakati huo kwa saa 2:03:23.