Mwanariadha Kipsang Korir aanguka na kufariki baada ya mbio nchini Cameroon

Baada ya kuvuka mstari wa mwisho, mwanariadha huyo wa Kenya alianguka kwa kile kilichoshukiwa kuwa mshtuko wa moyo.

Muhtasari
  • Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Cameroon, Kipkorir ambaye alikuwa akishiriki katika toleo la 29 la Mbio za Matumaini za Mount Cameroon, aliaga dunia huku akirejeshwa.
Mwanariadha Charles Kipsang Kipkorir
Image: KWA HISANI

Siku chache baada ya ,mwanariadha Kiptum kuzikwa,Wakenya waliamka na kusikia habari nzito Jumapili baada ya kujua kwamba mwanariadha Charles Kipsang Kipkorir alianguka na baadaye kufariki muda mfupi baada ya kumaliza mbio za ushindani nchini Cameroon Jumamosi, Februari 24.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Cameroon, Kipkorir ambaye alikuwa akishiriki katika toleo la 29 la Mbio za Matumaini za Mount Cameroon, aliaga dunia huku akirejeshwa.

Mwanariadha huyo alikuwa ameongoza wakati wa mbio hizo, kabla ya kuanza kupunguza kasi baada ya kupata matatizo, mita tu hadi mstari wa kumaliza.

Kipkorir baadaye angemaliza katika nafasi ya 16 kulingana na Gavana wa Cameroon Bernard Okalai Bilia.

Baada ya kuvuka mstari wa mwisho, mwanariadha huyo wa Kenya alianguka kwa kile kilichoshukiwa kuwa mshtuko wa moyo.

Madaktari waliokuwa katika hali ya kusubiri katika Uwanja wa Molkyo walitoa huduma ya kwanza ili kumtuliza mwanariadha huyo wa Kenya kabla ya kukimbizwa katika Hospitali ya Mkoa ya Buea.

"Hatuwezi kusema ni nini hasa kilitokea. Tunaweza kuamini kwamba ni kitu kama mshtuko wa moyo," Bilia alisema muda mfupi baada ya kifo cha Kipkorir kuthibitishwa.

“Tulifahamishwa kuwa alipokuwa anaenda kuchukua zawadi yake, alianguka na kuzimia. Walimbeba na kumpeleka Hospitali ya Mkoa, tayari alikuwa ameshafariki dunia.”

Kipkorir alikuwa nyota wa hafla hiyo, baada ya kuwa mwanariadha wa kwanza wa kigeni kujiandikisha kwa mbio za mlima za Cameroon, mashindano kongwe zaidi ya riadha ya kimataifa barani Afrika.

Wakati wa kifo chake, Kipkorir alikuwa na umri wa miaka 33 na katika kilele cha kazi yake.

Kipkorir alikuwa ameshiriki katika mbio nyingine kabla ya kujumuisha; Bali Marathon, Kuala Lumpur Marathon na Casablanca Nusu Marathon.

Kifo chake kilijiri wiki mbili tu baada ya Kenya kumpoteza mshikilizi wa mbio za marathon za Dunia Kelvin Kiptum kupitia ajali ya barabarani.