Jack Wilshere arejea kufanya mazoezi na Arsenal

Mchezaji huyo alichezea klabu hiyo kwa zaidi ya mwongo mmoja.

Muhtasari

•Wilshere ambaye aliachiliwa huru na klabu ya Bournemouth mwezi Mei alishirikishwa na Arsenal kwenye kipindi cha mazoezi kwa mara ya kwanza tangu mwaka wa 2018 siku ya Alhamisi.

Image: ARSENAL

Mchezaji Jack Wilshere amerejea katika klabu yake ya zamani Arsenal kwa minajili ya kufanya mazoezi baada ya kuwa bila klabu kwa kipindi cha miezi mitano.

Wilshere ambaye aliachiliwa huru na klabu ya Bournemouth mwezi Mei alishirikishwa na Arsenal kwenye kipindi cha mazoezi kwa mara ya kwanza tangu mwaka wa 2018 siku ya Alhamisi.

Hata hivyo kufikia sasa hakuna mipango zaidi ya kushirikisha kiungo huyo wa kati mwenye umri wa miaka 29 kwenye mechi.

Mkufunzi wa miamba hao wa London Mikel Arteta alisema kuwa Wilshere aliruhusiwa kushiriki mazoezi na klabu yake ya zamani ili aweze kujiweka katika hali nzuri ya mwili na kisaikolojia.

"Tunataka kusaidia Jack anapojitayarisha kwa hatua hiyo nyingine. Tunataka kumsaidia kujiweka sawa kimwili na kisaikolojia" Arteta alisema.

Wilshere anatazamia kuwa kocha miaka ijayo na Arsenal imejitolea kumsaidia katika matayarisho ya hatua hiyo.

Arteta alisema kuwa raia huyo wa Uingereza atasalia kwenye klabu ya Arsenal kwa kipindi ambacho hakijathibitishwa na ataendelea kufanya mazoezi na wachezaji wa klabu hiyo.

Wilshere aliondoka Arsenal mnamo Mei 2018 baada ya mkataba wake kuisha. Mchezaji huyo alichezea klabu hiyo kwa zaidi ya mwongo mmoja.