EPL 2021/22: Matokeo ya raundi ya 13, Hali ilivyo kwenye jedwali

Muhtasari

•Mechi kati ya Burnley na Tottenham iliahirishwa kwa sababu ya barafu iliyokuwa imeanguka uwanjani Turf Moor.

Image: PREMIER LEAGUE

Michuano ya EPL iliingia katika raundi ya 13 wikendi iliyotamatika huku mechi 9 zikichezwa katika nyanja mbalimbali Uingereza Jumamosi na Jumapili.

Wanabunduki walikaribisha Newcastle ugani Emirates katika mechi ya ufunguzi ambapo waliandikisha ushindi wa 2-0 na kuboresha nafasi yao ya kuingia nne bora. Washambulizi wachanga, Bukayo Saaka na Gabriel Martinelli walisaidia Arsenal kupata ushindi huo.

Mechi tatu zaidi zilichezwa Jumamosi mwendo wa saa kumi na mbili jioni.

Liverpool waliwika ugenini dhidi ya Southampton kwa kuwalaza mabao manne bila jawabu. Mabao mawili ya mshambulizi Diogo Jota pamoja na mabao ya Virgil Van Dijk na Thiago yalifanikisha ushindi huo.

Crystal Palace walipoteza 1-2 nyumbani dhidi ya Aston Villa huku mechi kati ya Norwich na Wolves ikiisha sare ya 0-0.

Brighton walikaribisha Leeds katika mechi ya mwisho siku ya Jumamosi ambapo dakika 90 za mchuano huo hazikushudia bao lolote.

Mechi ya kwanza siku ya Jumapili ilikuwa kati ya Brentford na Everton ambapo wenyeji Brentford waliandikisha ushindi wa 1-0.

Leicester walichapa Watford 4-2 nyumbani kupitia mabao ya Jamie Vardy (2),  James Maddison na Ademola Lookman huku Joshua King na Emmanuel Dennis wakifungia Watford.

Manchester City waliwaonyesha West Ham makali yao kwa kuwalaza mabao 2-1. Ikay Gundogan na Fernandinho ndio walifungia City huku Manuel Lanzini akifungia West Ham bao la pekee.

Mechi iliyokuwa imesubiriwa kwa hamu na ghamu kati ya Chelsea na United iliisha sare ya 1-1. Mashetani wekundu ndio walitangulia kufunga kupitia bao la Jadon Sancho katika dakika ya 50 huku Jorginho akisawazishia Chelsea katika dakika ya 69 kupitia mukwaju wa penalti.

Mechi kati ya Burnley na Tottenham iliahirishwa kwa sababu ya barafu iliyokuwa imeanguka uwanjani Turf Moor.

The Blues wanaendei wanaongoza jedwali na pointi 30, City ni ya pili na pointi 29, Liverpool ya tatu na pointi 28 huku West Ham ikifunga nne bora na pointi 23.

Nafasi tatu za mwisho zimekaliwa na Burnley (9), Norwich (9) na Newcastle (6),