Nyumba ya Kamara yalindwa na polisi baada ya kukosa penalti

Muhtasari

• Mshambulizi huyo wa zamani wa Norwich City na Middlesbrough bado hajazungumza lolote kuhusu kutumwa kwa polisi.

• Nyumba ya Kamara mjini Freetown ililengwa baada ya Sierra Leone kupoteza mchezo huko Limbe 1-0, na kuwaweka nje ya michuano hiyo.

• Polisi wa Sierra Leone - kama taasisi ambayo iko makini sana - walipata taarifa za kijasusi kuwa vijana wenye hasira walitaka kushambulia nyumba yake.

Nyumba ya mshambuliaji wa Sierra Leone Kei Kamara bado iko chini ya ulinzi wa polisi baada ya mshambuliaji huyo kukosa penati dhidi ya Guinea ya Ikweta kwenye michuano ya AFCON nchini Cameroon.

Nyumba ya Kamara mjini Freetown ililengwa baada ya Sierra Leone kupoteza mchezo huko Limbe 1-0, na kuwaweka nje ya michuano hiyo. Kama Kamara angefunga, ingewezekana wangepata sare ambayo ingewawezesha kupita.

"Ninaweza kuthibitisha kwamba polisi bado wapo katika nyumba ya Kei Kamara ili kuilinda dhidi ya vijana waliochukizwa na ambao hawana furaha kwa sababu alikosa penalti dhidi ya Equatorial Guinea," naibu mkuu wa polisi wa Sierra Leone aliambia BBC Sport Africa.

"Polisi wa Sierra Leone - kama taasisi ambayo iko makini sana - walipata taarifa za kijasusi kuwa vijana wenye hasira walitaka kushambulia nyumba yake na tukaamua kwenda nyumbani hata kabla ya mechi kumalizika."

"Tunajua kilichompata Umaru Bangura miaka michache nyuma, kwa hivyo tuliamua kuwa waangalifu."

Hii ilikuwa ni kumbukumbu ya nahodha wa timu hiyo, ambaye nyumba yake ilipigwa kwa mawe baada ya pia kukosa penalti , katika dakika za majeruhi wakati wa mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia 2022 dhidi ya Liberia.

Polisi waliongeza kuwa "hakuna madhara yoyote" kwenye nyumba ya Kamara na "vijana katika eneo hilo wanashirikiana nasi."

Mshambulizi huyo wa zamani wa Norwich City na Middlesbrough bado hajazungumza lolote kuhusu kutumwa kwa polisi.